Wasomi walaani mauaji ya Waislamu Mwembechai

Wasomi Waislamu kutoka taasisi za elimu ya juu za Tanzania wamelaani mauaji ya Waislamu yaliyofanywa na
jeshi la polisi katika maeneo ya Msikiti wa Mwembechai hapo Aprili 13, 1998.

Wasomi hao pia wameshangazwa na hatua za chama tawala (CCM) na Serikali yake kuwapongeza wauaji. Vile
vile Waislamu hao waliisihi Serikali kuunda tume huru ya kuchunguza mauaji na kuacha uonevu wa kuwanyima
dhamana watuhumiwa, ambao wengi wao ni wagonjwa, kwa visingizio ambapo wamedai havina msingi
wowote.

Sambamba na hayo, wasomi hao walimpongeza Bwana Kitwana Kondo Mbunge wa CCM jimbo la Kigamboni
kwa kuwajibika kwake kama Muislamu na pia kama Mtanzania, kuiambia wazi Serikali juu ya chuki iliyonayo
dhidi ya Waislamu.

Wasomi hao waliyasema hayo katika sherehe za kuadhimisha mwaka mpya wa Kiislamu, 1419 na kuwaaga
wanaomaliza masomo yao katika muhula huu wa masomo.

Sherehe hizo zilifanyika Mei 23, mwaka huu katika Chuo cha Maendeleo ya Uongozi (IDM) cha mjini
Morogoro na kuhudhuriwa na wasomi Waislamu kutoka chuoni hapo, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo
Kikuu cha Sokoine, Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo cha Uhasibu (DFA) cha Dar es Salaam na
Sekondari za Dar es Salaam na Morogoro

Katika sherehe hizo ziliichangwa shilingi 80,870/- kwa ajili ya kulipia gharama za kuendesha kesi
zinazowakabili Waislamu kutokana na tukio la Mwembechai.