ISISTAWISHWE DHANA KWAMBA: Serikali inapenda Waisilamu wafe

 

Mheshimiwa Kitwana Kondo (MB) ametoa ufafanuzi kwamba anachofanya sio kutafuta umaarufu bali
kutekeleza wajibu wake na haki yake ya kuishauri Serikali na Chama chake CCM, iache kutojali mambo
yanayowahusu Waislamu.

Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake Mei 27; Mh. Kondo alisema kwamba kutokujali kwa
Serikali katika masuala ya Waislamu kunatoa tafsiri kwamba bila shaka Serikali haiwapendi Waislamu.

Akitoa mfano alisema kwamba watu walio ndani wengi ni wagonjwa, wengine wazee na wameshakaa ndani
kwa zaidi ya miezi mitatu na mmoja kesha kufa. Katika mazingira hayo alisema kwamba dhana ipo kwamba
Serikali inafurahia hivyo; kwamba wafe mmoja mmoja!!

Kuhusu kile kinachoitwa kwamba ni kashfa dhidi ya dini nyingine Mhe. Kitwana Kondo alikariri kauli yake ya
Mei 21; kwamba Serikali isiyo na dini inafanya kosa kuwashitaki watu kwa sababu ya imani yao. Alisema
kuwashitaki watu kwa kusema maneno yaliyoko ndani ya Qur’an ni sawa na kusema kwamba Qur’an ni kitabu
cha uchochezi ambacho inabidi chenyewe na Uislamu wenyewe upigwe marufuku.

Mhe. Kondo alishangaa na kuhoji Serikali inaposema kashfa kwa dini nyingine. "Dini gani?’ Wakati Maaskofu
wenyewe wanasema Muislamu kusema Yesu si Mungi si kosa wala si kashfa!

Akithibitisha kwamba wanayosema Waislamu yapo ndani ya Qur'an yao, Mheshimiwa Kitwana Kondo akiwa
na Msahafu wa tafsiri ya Qur'an alizinukuu aya zifuatazo:

Kwa yakini wamekwisha kufuru waliosema: "Mwenyezi Mungu ni Masihi bin Maryamu. (5:17). Bila shaka
wamekufuru wale waliosema; Mwenyezi Mungu ni Masihi (Isa) bin Maryamu. (5:72).

Kwa hakika wamekufuru wale waliosema: "Mwenyezi Mungu ni mmoja katika (wale waungu) watatu. (5:73)

Masihi bin Maryamu si chochote ila ni Mtume (tu). (Na) bila shaka Mitume wengi wamepita kabla yake. (5:75)

Na kwa (ajili ya) kusema kwao: "Sisi tumemuua Masihi Isa mwana wa Maryamu Mtume wa Mungu", hali
hawakumwua wala hawakumsulubu... (4:157).

Kuhusu suala la dhamana Mhe. Kondo alisisitiza kwamba ni Serikali inayozuia dhamana na wala sio
Mahakama. Alisema kwamba ni Serikali iliyoshitaki na ndiyo inayotoa hoja Mahakamani kuzuia dhamana.
Kwahiyo ameitaka Serikali iache kubabaisha kwa kusema kesi ipo mahakamani.

Aidha Mhe. Kitwana Kondo amerejea kauli yake kwamba Serikali ilifanya makosa kwa Polisi wake kuvamia
na kuvunja msikiti. Lakini pia akasema kwamba Serikali ilichangia vurugu za Mwembechai kwa kitendo chake
cha kumkamata Bw. Magezi msikitini kukiwa kumejaa watu

Maelezo haya ya Mhe. Kondo ameyatoa kufuatia maelezo yaliyotolewa na Serikali na baadhi ya taasisi juu ya
yale aliyozungumza na waandishi wa habari Mei 21.