YARABI WAHUKUMIE MWEMBE CHAI
1. Bismillahi jinale, ndilo ninalo anzia,
Rahmani vilevile, waakherana dunia,
Mfalme wa milele, mwenye sifa zote pia,
Yarabi ishushe rehma, maovu kutulipia.
2. Yarabi Mola Mwenyezi, mwengine hatatokea,
Muumba jua na mwezi, mchana usiku pia,
Mwenginewe hachomozi, katika yetu dunia,
Yarabi tuhukumie, mwembechai kuonewa.
3. Yarabi waangamize, laana kuwashushia,
Na kisha watokomeze, macho yao kupofoa,
Mengine wasiweze, walilolikusudia,
Yarabi uwape maradhi, wateseke na dunia.
4. Yarabi Mola jalali, takabali yangu dua,
Uwape adhabu kali, motoni wende ingia,
Waipate idhilali, kama waliotangulia,
Rabi lete masusura, Mwembe chai kuiokoa.
5. Hilolao kongamano, utawala ulioko,
Ulete mfarakano, tena wala wasiweko,
Yaondoshe mapatano, patokee machafuko,
Ninainua mikono, nakuombea juu yako.
6. Lete utawala mwema, tushike amri zako,
Lile ulilolisema, tufate hilo tamko,
Nchi pate salama, iwache misukosuko,
Kiongozi muadilifu, yarabi tuoneshee.
7. Mungu hushindwi na kitu, utakalo litakuwa,
Mungu wala si mwenzetu, hakuzaa hakuzaliwa,
iokoe nchi yetu, dini yetu kuonewa,
Waumini Mwembechai, Balaa waondoshea.
Bi, Batuli Ahmed.M.Al-Amary
S.L.P. 4 Pangani Tanga.
|
NICO NIMESHASILIMU
Bismilah ya kwanza, ya pili Arahamani,
Bora nishukuru kwanza,kwa yule yule Manani,
Alonifanya kuweza, kukaa hapa kitini,
Ndugu zangu eleweni, Nico nimeshasilimu.
Sasa nimejieneza, vifaa vyote mezani,
Jambo ninaloliwaza, taarifa kuwapeni,
Si vizuri kunyamaza, bora niwajulisheni,
Ndugu zangu eleweni, Nico nimeshasilimu.
Shairi naliandika, mnielewe makini,
Kwani litatawanyika, kote kote duniani,
Taarifa zitafika, Bara hata kule Pwani,
Ndugu zangu eleweni, Nico nimeshasilimu.
Barua ningeandika, hata kama ishirini,
Wengi watanung’unika, waseme nimewahini,
Ndugu watakasilika, waniulize kwa nini?
Ndugu zangu eleweni, Nico nimeshasilimu.
Barua hamtoenea, ndugu jamaa jirani,
Jambo niloonelea, taarifa niwapeni,
Shairi kuwatungia, mlisome gazetini,
Ndugu zangu eleweni, Nico nimeshasilimu.
Mwezi wa kumi na mbili, wiki ya mwisho jamani,
Ndivyo nilivyo salimu, mbele ya yeye Manani,
Kuwa nimeshastakimu, ule wangu uumini,
Nico nimeshasilimu, sasa naitwa Nassoro.
Mimi sasa Isilamu, nawaomba eleweni,
Naomba msilaumu, mkauliza kwa nini?
Kwangu mimi kusilimu, nisiwe mashindanoni,
Nico nimeshasilimu, sasa naitwa Nassoro.
Jina la sasa Nassoro, naomba nitambueni,
Jina lisilo kasoro, kwenye hii yetu dini,
Jina la Nico kiporo, kutumia sitamani,
Nico nimeshasilimu, sasa naitwa Nassoro.
Kusilimu si ajabu, hilo kwanza eleweni,
Kusilimu ni thawabu, aliyanena Manani,
Msijenipa adhabu, kwa maswali ya kwa nini?
Nico nimeshasilimu, sasa naitwa Nassoro.
Nico mimi kusilimu, msiseme punguwani,
Ninaakili timamu, hilo nawajulisheni,
Msinione dhalimu, mkanitenga jamani,
Nico nimeshasilimu, sasa naitwa Nassoro.
Nassoro ni jina langu, naomba lizoeeni,
Barua zilizo zangu, Nassoro niandikeni,
Box na simu zangu, zile zile za zamani,
Nico nimeshasilimu, sasa naitwa Nassoro.
Kuna jambo la muhimu, bora niwajulisheni,
Kuna wazee muhimu, bora niwatajieni,
Ayub ndiyo Imamu, na Magwila sikieni,
Nico nimeshasilinu, sasa naitwa Nassoro.
Mahali kibra teni, ni pale msikitini,
Aggrey mtaani, asiyepajua nani?
Shahada ninayo ndani, ushahidi si utani,
Nico nimeshasilimu, sasa naitwa Nassoro.
Nassoro jina halisi, mimi ni wenu mtani,
Mimi sikai Masasi, Chalinze ndiyo nyumbani,
Kuandika sasa basi, nawahi msikitini,
Nico nimeshasilimu, sasa naitwa Nassoro.
NASSORO GOHA, DAR ES SALAAM. |