Jumuia ya wanafunzi Waislamu wa vyuo na sekondari mkoani Arusha (TAMSA), wanaungana na wanafunzi wenzi wao wa nchi nzima katika kuunga mkono kauli iliyotolewa hivi karibuni na Mhe. MB. Kitwana Kondo kwa waandishi wa habari.
Pamoja na mambo mengineyo waliyoongea kuhusu kuimarisha Uislamu na elimu yao, walihitimisha kwa kuyalaani mauaji ya Waislamu yaliyofanywa na polisi wa serikali ya CCM katika Msikiti wa Mwembechai.
Walisema, kamwe hawataungana na serikali katika kupongeza mauaji kwa namna yalivyofanyika kinyama.
Walisisitiza kuwa mauaji ya namna ile yakifanyika kwa Waislamu ama kwa mtanzania yeyote yanastahili kulaaniwa vikali kwa kuwa yanalet utamaduni mpya katika jamii yetu.
Pia walidai kuwa, kijana Chuki Athumani anayeendelea kuugulia hospitalini kutokana na majeraha ya risasi za polisi, amedhulumiwa haki yake ya kuwa na afya njema, na haki yake ya kuendelea kupata elimu na pia amehatarishiwa maisha yake na wale wanaopaswa kulinda uslama wa raia wa nchi hii.