Joka la Mdimu -14

GARAY KWACHA

AMANI aliendesha gari lake taratibu pembeni kaketi tajiri wake Shiraz Bhanj. Baada ya muda si mrefu alifika mbele ya jengo la Hazina Kuu. Ilitimia saa tatu kamili na sehemu yote ya maegesho magari madogo mbele ya jengo hilo ilijaa. Amani anapitisha macho huku na kule aliona Mzungu mmoja akiingia ndani ya Toyota Cressida na kurudi kinyume. Upesi Amani aliingia na kuegesha gari lake katika nafasi ile iliyoachwa wazi.

"Amani", Shiraz Banj aliita huku akifungua mlango wa mbele wa kushoto mkononi kashika mkoba wake.

"Naam tajiri", aliitika.

"Subiri baba. Iko appointment na Kurugenzi ya Foreign Exchange mara moja".

"Ndiyo tajiri", alijibu huku akimwangalia Bhanj alivyopata shida kutembea kuelekea ngazi za kwenda ndani ya ofisi yenyewe. Alivaa suruali nyeupe kumbwaya na shati jeupe nalo kumbwaya lakini bado lilionyesha tumbo lake kubwa ambalo lilitetemeka kuujibu kila mguu ulioinuliwa na kutua ardhini kwa kishindo. Alipozikaribia ngazi zenyewe alipania suruali yake. Amani alimwangalia akipanda kwa takilifu kuu, mkono wa kulia alipunga mbele na nyuma kumpa msimamo mzuri ilihali ule wa kushoto ulikuwa umebanwa juu ya nyonga chini ya jitumbo lenyewe.

Bhanj hakuwa na mazoea makubwa ya kwenda kwa Mkurugenzi wa Fedha za Kigeni. Yeye hakuwa na tatizo la kupata fedha za kigeni. Alijigamba kuwa ana dola na pauni nyingi hata kuzidi benki yenyewe. Namna alivyozipata ilikuwa siri yake. Ila Amani alikua anajua kuwa mojawapo ni kwa njia ya magendo. Hii leo alikuwa na masuala muamala mahususi wa utaka kusafirisha bidhaa zake kwenda Sweden na Ubelgiji. Haja yake ilikuwa kupata kibali cha kutekeleza shughuli hiyo.

Idara ya Fedha za Kigeni ilikuwa katika ghorofa ya juu kabisa. Gray Kwacha alikuwa ndiye Mkurugenzi wake chini yake akiongoza wafanyakazi wasiopungua hamsini.

Gray Kwacha alikuwa kinyonga: saa ana furaha, saa hana. Leo ana hili, kesho lile. Nyendo zake nyingi zilitiliwa mashaka. Hakuwa wa kuvutia kwa umbo, macho makali, pua fupi pana, midomo yenye mbalanga, alishabihi zaidi jambazi wadhifa wake. Mjuzi wa hilo aliugubika walakini huo katika mavazi na kipato chake. Maradhi yake makuu ilikuwa anasa mintaarafu wanawake.

Ofisi yake ilikuwa pembeni kwa upande wa mashariki.

Shirazi Bhanj alichukua zaidi ya dakika kumi kufika kwa Katibu wa Gray Kwacha. Alifungua mlango bila ya kugonga. Pua zake zikalakiwa na riha ashafu ya manukato. Ana kwa ana naye kiliketi kipande cha mwanamke kilichosimama macho laini kumlaki. Mtu angedhani labda usiku kucha hakuliangua lepe la usingizi kwa jinsi mboni zilivyolainika.

Bhanj alitembea juu ya zulia jekundu. Makubadhi yake yalizama ndani ya manyoya marefu laini ya zulia hilo. Madirisha ya vioo ya chumba hicho yalikuwa yamefungwa kusaidia mashine ya kupooza hewa. Lakini mapazia yake makubwa mazito yalivutwa kila pembe ya dirisha yakawa mithili ya majora mawili mekundu yaliyoegemezwa pembeni humo.

"Jambo bibi?" Bhanj alisalimia akitabasamu kwa 'chati'.

"Karibu", alijibu yule banati.

"Bana kuba iko?"

"Ndiyo! Subiri ana mgeni mwingine", alijibu akiendelea kupiga kompyuta bila ya kuinua macho.

Bhanj alitupa macho huku na kule, kwa muda yakuta juu ya saa yake, kabla ya kuangalia juu ya makochi mekundu yaliyotengenezwa kwa mbao za mninga. Bhanj alijitupa na kuketi katikati ya kochi moja, kainua mguu mmoja huku mwingine kule, mkono huku na mwingine huko.

Kote kukawa kimya isipokuwa kwa sauti ya mashine ya kiyoyozi na kompyuta iliyokuwa ikisalimu amri ya vidole vya yule msichana Katibu.

Kimya kimya. Wageni wengine wawili, mmoja Mwarabu na mwingine Mzungu, walifika hapo kwa mpigo na kufuatiwa na mrembo mmoja aliyevaa sare ya shirika la Ndege la Ethiopia. Alikuwa mrefu wa kuvutia vigumu kusimulia. Kila alichokivaa kiliongeza haiba yake.

Yule Katibu hakupendezwa na ujaji wa mrembo yule. Naye, kuambiwa kuwa Kwacha alikuwa na mgeni mwingine, alisimama hapo kwa muda kama asubiriaye kuamua kuketi, kusimama au kuondoka. Lakini kabla ya kukata shauri mlango ulifunguliwa akatokea mwanamke mmoja akifuatiwa na Gray Kwacha.

"Ah! Leila!" alimsalimu kwa furaha, "Karibu ndani tafadhali". Alifungua mlango wazi zaidi aingie huku akiwapitisha macho ya haraka wale wageni wengine waliokuwa wakisubiri. Wageni walibakia wakitazama huku wakifaidi zawadi ya manukato bora aliyowaachia Leila.

Leila alikuwa mpenzi mpya wa Gray Kwacha. Alikutana naye ndani ya ndege alipokuwa akienda London kuhudhuria moja ya vikao vyake vingi mintaarafu na miale amle ya fedha duniani. Mawasiliano yao baada ya hapo yalikuwa ya juu juu tu wakati ndege ya Shirika la Ndege la Ehiopia ilipotua jijini Mindule kabla ya safari zake za kimataifa. Hivyo alipomuona tu damu ilimwenda kasi, na mate mazito yakamjaa kinywani. Akaona kheri amfichulie mpango wake ambao aliubuni siku ayami. Baada ya mazungumzo mafupi alimtobolea.

"Lini utakuwa na off?"

"Sio hivi karibuni. Lakini nafikiri baada ya majuma mawili".

"Kwani kuna nini?" aliuliza akielewa fika alichokuwa kikipita ndani ya fikra zake.

"Nilitaka tupate wasaa".

"Wasaa?" alijifanya kushangaa.

"Ndiyo!" Kwacha alisisitiza.

"Si huu tunao?" alisema akikaza macho huku akijizuia kucheka. Lakini Gray Kwacha alikuwa mwingi wa habari na alimjua kaa alipo! Kazi yake ikawa kumchokoa taratibu akisubiri aliko atoke amshambulie.

"Wewe wadhani watosha?"

"Sana", alicheka huku macho yake yakilengalenga machozi. Hiyo ilikuwa silka yake. Daima utando mwembamba wa machozi uliengaenga macho yake na kuamsha jaza isio kifani nyoyoni mwa marijali. Sauti yake mithili ya chiriku ilichochea hisia hizo. Kasi ya mapigo ya moyo wa Kwacha iliongezeka mara mbili. Akajiuliza lini ataacha tabia yake ya kupenda wanawake wazuri? Akaitafuta sababu iliyomletea kigonjwa hicho na dawa mjaarabu ya kukiondoa. Zamani alifikiria kosa walilifanya wazazi wake kumwoza mwanamke ambaye hakuvutia. Hata hivyo yeye alimkubali mwenyewe. Basi kama ni hivyo labda alioa mapema mno wakati ambapo alikuwa hajakutana na vipande hasa vya kutazamwa na kutazamika. Lakini zote hizo hazikuwa sababu za kweli. Mwanzo alifikiri ujana. Lakini sasa alikaribia miaka hamsini. Nyumbani hakuwa na raha na mkewe wala watoto wake: kila siku visingizio. Akabuni mbuni nyingi zaidi za kujipatia fedha kukidhi anasa zake. Kwacha alishusha macho kumtazama Leila na kutoa rai.

"Twende kuwinda wakati wa off yako?"

"Sijawahi kuwinda! Naogopa".

"Huna haja ya kuogopa".

"Wapi?"

"Kwale. Mbuga ya wanyama ya Taifa".

"Nimewahi kuisikia".

Kiliwashtua kimya kifupi Leila akiangalia saa yake ya dhahabu, akakunja miguu kujitayarisha kuondoka. Moyo wa Kwacha ulimjaa kwa majonzi.

"Kwani ndege inaruka saa ngapi?" aliuliza.

"Baada ya saa mbili".

"Sasa unakwenda wapi?"

"Hilton".

"Nikusindikize?"

"Hapana! Nisipoteze muda wako".

"Kazi haishi".

"Nimekusamehe".

Gray Kwacha alituliza jazba yake alipowaza namna ambavyo angewapita akina Bhanj pale nje. Mwisho, shingo bawani, akasema "Sasa tumekubaliana kwenda kuwinda?"

"Ni confirm nikifika tena hapa".

Gray Kwacha alikuwa taabani, mikono mfukoni, akaona aibu hata kusimama kumtoa Leila mlangoni.

"Bye!" aliaga alipofika mlangoni na kutabasamu.

"Bye!" Leila alimjibu.

Ikawa zamu ya Shiraz Bhanj. Akajikokota huku tabasamu kalivaa usoni. Bhanj alifika na kuketi mbele ya meza ya Gray Kwacha.

"Wasemaje Mister Bhanj".

"Mambo ote nayo veve bana".

"Nini ile permit yako siyo?"

"Diyo".

Gray Kwacha aliinamia kidogo upande wa kushoto akavuta dawati. Alipekuwa katarasati za humo ndani kwa muda mfupi mpaka alipozipata zile hati za Bhanj. Alizichomoa ratatibu, akaziangalia vizuri kwa muda. Bhanj aliketi moyo ukimwenda mbio macho kayafotoa, meno kayakenua, uchu wa kipato zadi umeshtadi.

"Chukua" Gray Kwacha alisema. Bhanj alizipokea kwa mikono miwili akitetemeka.

"Sante bana".

"Umefurahi?"

"Ndiyo! Hata veve tafurahi".

"Wapi! Weye Mhindi mchoyo kweli kweli"!

"Sikia!" Bhanj alishusha sauti. "Tayari mimi nakwishaveka dola alfu laki moja dani ya akaunti yako Geneva".

"Lini?" Kwacha aliuliza kwa shauku akiacha kuegamia kiti chake cha mzunguko na kusogea mbele kulipata kila neno la Bhanj.

"Tangu viki napita", akaendelea tena. "Kwani veve hapana uliza?"

"Nchi hii imeharibika. Siwezi kupiga simu wala telex. Vidola vichache tu itakuwa kelele mtindo mmoja". Lakini akaendelea "usijali, kuna safari ya Rome na London baadaye mwezi huu".

"Basi naweza pitia Geneva aone. Mimi nakip promise".

"Najua".

Kulipita kimya kifupi na Gray akaulizia, "utakunywa kahawa?"

"Hapana. Moyo wangu bovu. Sauri ya pressure" alisema huku akipigapiga kifua kwa kiganja cha kulia.

"Chai?"

"Hapana. Sukrani". Kilipita kimya kingine kabla Gray kuuliza, "Kuna mali mpya gani dukani kwako?"

Bhanj alijawa fahari akajibu, "Kila kitu. Iko suti mpya, guo mama na toto, perfume, Martini, Martel na kila aina ya brandy na whisky".

Ghafla fikra za Kwacha ziliruka kwa Leila. Alivuta pumzi kwa nguvu na kuhema kwa kishindo. Aliinua macho yake pale mezani kumtazama Bhanj. "Weka perfume nzuri aina mbili".

"Taweka pacorabane na Marcho Polo".

"Na kitambaa kimoja kizuri cha gauni".

"OK", alijibu huku akisimama kuaga. Kwacha naye alifanya hivyo huku akizungusha kiti chake kupata nafasi ya kutoka. Alimsogelea karibu Bhanj akanong'ona, "Sasa nitakuletea mali yangu unisafirishie".

"Ooo! Iko bei kuba sana Arabuni siku hizi. Ninayo order kuba".

"Lakini safari hii nina consignment kubwa, karibu pembe mia moja, hivyo angalia sana".

Kila mmoja alibaki kimya. Walisimama hapo wakitazamana kutafutana undani. Kwa muda ikapita tuhuma baina yao. Lakini kati yao palikuwa na mtangamano ulioletwa na kuhitajiana kwao.

Alipotoka Bhanj waliingia tena wageni wengine ambao hawakuchukua muda mrefu.

Saa sita na robo Gray Kwacha alijiandaa kutoka. Taratibu alitembea na kupiga miayo. Alisimama kunako madirisha ya mashariki, akiangalia nje. Miti mizuri ilinesa kufuatisha upepo huku ikidondosha majani machache ya njano. Gray Kwacha aliangalia uzuri wa miti ile, majani yake kijani ya kukoleza. Lakini hakuna lisilo mwisho. Hata miti nayo huzeeka na kufa kama yalivyoashiria yale majani ya njano yaliyopukutika baada ya kumaliza uhai wake wa kuitengenezea chakula miti ile. Aligeuka kuelekea mlangoni na kutoka. Lakini katika ofisi ya Katibu wake akakutana na Josephine ambaye alimuuliza, "Gray unatoka?"

"Nilikuwa najiandaa kufanya hivyo. Karibu". Alisema huku akifungua tena mlango wa ofisi yake.

Katibu wa Gray Kwacha alimtazama mkuu wake akistaajabu namna alivyoweza kukaidi kuwahudumia wengine na vile alivyolainika mbele ya wasichana akawa kama jani la mboga. Gray Kwacha aliwahi kupigana kumgombea Josephine. Sio hivyo tu, mke wake Kwacha aliwafumania nyumbani kwake. Karaha hiyo ilizusha malau na vipijo. Kama nyati aliyejeruhiwa mke wake Kwacha alimrarua Josephine na kumtoa nje uchi ambako alitupiwa nguo zake. Bahati nyumba yenyewe haikuwa mtaa wa wengi au la angepata izara isiyo kifani. Hata hivyo athari haikukosa. Hadi leo ngeu ya mshono katika mdomo wa chini ilionekana japo kwa kuitazama kwa makini. Baada ya mkasa ule walimwengu wakatabiri kufungwa kwa ukurasa wa mahaba baina ya Josephine na Kwacha. Ila walisahau kwamba mwenye lake haliachi.

"Keti Joy", Kwacha alimkaribisha huku mwenyewe akijitadaza kwenye kiti chake, moyoni akijisema afadhali mawazo ya Leila yamtoke kidogo maana badala ya Hussein Hassan!

Unakunywa soda?"

"Namwogopa Katibu wako", Josephine alidhihaki.

"Ana nini?"

"Jibu alilonitupia lingekuwa mshale saa hizi marehemu".

"Umeanza mambo yako hivyo. Utakuwa lini?"

"Wataka niote ndevu za ulimi?" alijibu akitabasamu.

Josephine alikuwa ni ile aina ya wasichana wa mjini waliostahabu kusema chochote kilichowafurahisha. Siku za mwanzo silka hiyo ilimwudhi Kwacha lakini mtaka waridi sharti avumilie miiba.

"Mie nna njaa bwana", Josephine alilalamika.

"Sema nikupeleke ukale?"

"Ngoja kwanza nikueleze lililonileta". Kwacha aliegemea vizuri kiti chake na kumtazama vyema. Alikuwa msichana mweusi mwenye macho meupe makubwa yaliyozungukwa na kope ndefu. Josephine alikuwa na vichaka viwili vya nyusi ambavyo aghalabu alivitinda akabakiza mstari mwembamba, ushahidi wa nyusi hizo. Juu yake aliongezea kwa mstari mwingine wa rangi akitumia kalamu maalum ya risasi.

"Nakusikiliza". Kwacha alisubiri.

"Nataka kwenda London".

"Kufanya nini tena?"

"Kutembea".

"Wacha mzaha. Siku ulikuwa huko mwezi uliopita tu?"

"Nataka kwenda kufanya shopping ya harusi ya shoga yangu".

"Nani?"

"Pamela".

Sura ya kuvutia ya Pamela ilitanda machoni pa Kwacha. Akakumbuka hila alizozitumia kumpata Pamela. Lakini Pamela, kama mwanariadha stadi aliviruka viunzi vyote vya Kwacha. Kwacha alistaajabishwa na tabia ile ya Pamela. Mwanzo ilimchukiza lakini taratibu alianza kumheshimu.

"Pamela mwenyewe hajanieleza".

"Kanituma miye".

"Yeye anaogopa nini?"

"Wamtakia nini?" Josephine akapandisha sauti ya wivu. Kimya kifupi kilipita na Kwacha akauliza, "Kiasi gani? Cha kutosha kununua vitu vya harusi. "Kama poundi alfu sita hivi".

"Hizo fedha nyingi sana. Hatuna fedha za kigeni".

"Wasemaje?"

"Hakuna fedha za kigeni".

"Mbona nyie hamuishi safari, mwatujoki siye sio?"

"Safari zetu za kazi".

"Za kazi! Mwatufanya hatujui?"

"Lakini wewe si tulikwishakwenda Brussels pamoja?"

"Brussels, sio London".

"Basi mwache Pamela mwenyewe aje".

"Nyoo! Najua uliko! Baradhuli mkubwa! Huna haya?" alisema kwa hasira kidogo.

"Wacha wivu wako", Kwacha alimkatisha.

Kimya kirefu kilipita tena. Akakumbuka msemo 'nikune nikukune' lakini hatimaye akajibu, "Basi lete maombi yenu nitayapitisha".

Wote walisimama na kutoka kwenda hoteli ya Hilton kwa maakuli.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook