MAKALA

Lipumba kabwela Mwanza

Baba Kabwela UNO ni wimbo uliokuwa mashuhuri miaka ya hamsini mwishoni ukielezea tukio muhimu katika historia ya nchi hii, ambalo lilimchukua Mwenyekiti wa TANU Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hadi Umoja wa Mataifa kuelezea haja ya Watanganyika kujitawala wenyewe.

Walikuwa ni wasanii wa kabila la Kizaramo walioimba wimbo huo katika ngoma yao mashuhuri ya Mganda.

Wananchi kwa maelfu waliomiminika kumlaki Mwenyekiti huyo wa TANU hawakusita kuonesha furaha yao pale ndege iliyomchukua ilipokuwa ikitua katika uwanja wa ndege wa Dar.

Ilikuwa hoi hoi, shangwe na vifijo mitaa yote ya jiji la Dar es Salaam kufuatia kuwasili kwa Nyerere akitokea UNO. Ilikuwa safari ya kisiasa iliyozaa tukio kuu la mwaka 1961.

Mapokezi yaliyofanywa na chama cha CUF wiki hii yameelekea kuikumbusha historia hiyo pale wakazi wa Jiji walipofurika uwanja wa ndege wakiimba na kucheza wengine wakiwa wamejipanga barabarani kumlaki Profesa Ibrahim Lipumba akitokea mkoani mwanza ambako mkutano maalum wa chama cha CUF ulimteua kuwa mgombea wa kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ingawa mapokezi hayo hayakuwa yamepewa umuhimu na vyombo vya habari kulinganisha na ilivyokuwa kwa wagombea wa CCM, kwa siku tatu mfululizo miti na kuta mbali mbali jijini zilionekana kuwa na matangazo yanayotaarifu kuwasili kwa wagombea hao.

Kuanzia milango ya saa nne asubuhi, Mwandishi wa habari hizi alishuhudia makundi ya wananchi kando kando ya bara bara ya Nyerere kuelekea uwanja wa ndege.

Hadi kufikia saa sita za mchana msururu mkubwa wa watu ulionekana kujipanga kuanzia eneo la Kipawa hadi Uwanja wa Ndege ambako umati mkubwa wa watu ulijazana eneo lote la bustani lililoko nje ya jengo kuu la uwanja huo. Kutokana na msongamano wa watu, vijana wadogo walionekana kukwea miti ya uwanja huo kupata fursa ya kuona vyema kila tukio.

Makamanda wa ngazi za juu wa jeshi la polisi nchini hawakungoja taarifa kutoka kwa vijana wao, walifika wenyewe kushuhudia kile kilichoendelea katika mapokezi hayo.

Mkuu wa Jeshi la polisi nchini Bwana Omar Mahita akiwa na mkurugenzi wa upelelezi nchini bwana Adadi Rajab, Kamanda wa Polisi mkoa wa Dar es Salaam Bwana Alfred Gewe, mkuu wa upelelezi wa mkoa Bwana Said Mwema na makamanda wengine nao walikuwa sehemu ya uma uliofurika uwanjani hapo.

Matangazo ya awali yalifahamisha kuwa ndege iliyokuwa iwachukue wagombea hao ilikuwa ifike saa 5:30 asubuhi, hata hivyo yalitokea mabadiliko ya ghafla hali ambayo nusura izue mtafaruku kutoka wananchi hao ambao wengine walikwishajitoma ndani kuulizia ratiba ya ndege za siku hiyo.

"Msipomleta leo tutalala hapa hapa", ni baadhi ya matamshi yaliyokuwa yakitolewa na wafuasi hao huku wakisogelea mlango wa kutokea wageni.

Ndege aliyopanda Profesa Lipumba iliwasili kiwanjani hapo saa saba na dakika kadhaa mchana tukio lililoamsha shamra shamra kubwa zilizohusisha maonesho ya sarakasi kutoka kwa vijana waliokuwa wakisubiri kwa hamu kubwa.

Mayowe yalipasua anga mara tu mgombea huyo alipotokeza akiwa ameandamana na mgombea wake mwenza bwana Nassor Khamis wakisindikizwa na Mgombea wa Zanzibar Maalim Seif Shariff Hamad ambaye kwa mujibu wa msemaji mmoja wa CUF aliwasili jijini siku mbili kabla akitokea mikoa ya Mbeya na Iringa.

Patashika ya mapokezi hayo ilisababisha kijana mmoja ambaye hakufahamika jina lake kukanyagwa mguu na gari moja aina ya suzuki iliyokuwa ikirudi nyuma.

Msafara wa wagombea hao ulianza kuondoka taratibu uwanjani hapo huku maelfu ya watu yakisindikiza kwa nyimbo, vijana wakiwa wamezingira gari walilopanda wagombea hao.

Umati huo uliongezeka eneo la nje ya uwanja huo ambako uma mwingine mkubwa ulikuwa umejipanga kando kando ya bara bara ya Nyerere mbali ya wale walioshonana hasa kwenye magari ya wazi yaliyoegeshwa pembeni mwa bara bara hiyo yakisubiri kuunga nyuma ya waendao kwa miguu.

"Ameteremka! Ameteremka! CCM tumbo joto, wanatetemeka, wanaona homa", Lipumba huyo! Lipumba Huyoo, kaingia", ni miongoni mwa nyimbo zilizoimbwa na umati huo watu uliofunga bara bara nzima ya Nyerere.

Magari yaliyokuwa yakitokea eneo la mjini yalilazimika kuegeshwa pembeni kuupisha msafara huo uliokuwa ukitembea kwa taratibu kuelekea uwanja wa kidongo chekundu gerezani jijini.

Ilikuwa vigumu kuona mwanzo au mwisho kwa mtu aliyekuwa kati kati ya msafara huo uliotembea mwendo wa makumi ya kilometa.

Msafara huo ulijigawa ulipofika makutano ya bara bara za Mandela na Nyerere ambapo magari ya wazi yaliyojaa wafuasi na wapenzi wa chama hicho yalipita moja kwa moja kuelekea kidongo Chekundu wakati magari mengine yakiongozwa na Fuso lililotoa burudani ya aina yake yakiongozana na umati mkubwa wa watu waliotembea kwa miguu ulikata kona na kuingia Mandela Road ambako uliongezewa na umati mwingine uliokuwa ukisubiri kando ya barabara hiyo.

Msafara ukiwa na gari walilopanda wagombea ulikata kona nyingine eneo la Buguruni kuingia bara bara ya uhuru ambayo ilifungwa kabisa kwa magari mengine kupita.

Mwandishi alishuhudia watu waliosimama nje ya nyumba katika maeneo ya kwa Malapa, Ilala Bungoni na Amana wakipunga mikono. Wafuatiliaji wa mambo ya kisiasa wameyaelezea mapokezi hayo kuwa hayajapata kuonekana katika pilika pilika za kisiasa hapa nchini.

Toka saa saba za mchana ulipoanza msafari huo watembea kwa miguu waliwasili Uwanja wa Kidongo chekundu saa tisa na nusu alasiri kupitia bara bara ya Nyerere(Pugu Road), Mandela, Uhuru na Lumumba.

Mzee mmoja maarufu jijini akielezea hali aliyoishuhudia Kidongo Chekundu alisema aliifananisha na Mkutano mkubwa uliofanyika miaka ya hamsini katika viwanja mnazi mmoja.

"Mkutano huo ulikuwa maalum kumuunga mkono hayati mwalimu Nyerere baada ya baadhi ya wazee kuonesha wasi wasi juu ya muelekeo wake kisiasa ndani ya TANU", Mzee huyo aliwaeleza watu waliosimama pembezoni mwa uwanja huo.

Kivutio kikubwa kilikuwa Mzee aliyekuwa akipuliza tarumbeta akiongoza kikundi cha vijana waliokuwa wakizunguka mitaa ya jirani na uwanja huo wakati mkutano ukiedelea.

Aidha kulikuwa na kikundi cha vijana waliokuwa wakibebeshana gunia kubwa lililoandikwa maneno "mzigo wa madeni ya serikali ya CCM unawaumiza wananchi".

Akizungumza katika mkutano huo, Profesa Ibrahim Lipumba alisema amefarijika sana na moyo(spirit) wa kujituma na kujitolea ulioonesha na wananchi hao ambao alisema ni ishara njema ya "Ngangari" mwezi Oktoba.

Naye Mgombea wa kiti cha Urais Zanzibar Bwana Seif Shariff Hamad akiwasalimia wananchi hao, alisema umefika wakati kwa watanzania, bara na visiwani kuondokana na utawala wa CCM.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook