Elimu ya Dini ya Kiislamu kwa shule za Sekondari
 
Historia: Form One

Maana ya Historia

Kuna ugumu katika kueleza maana ya Historia kwa maneno machache, kama vile ilivyo kwa masomo mengine ya sayansi ya jamii. Ugumu huu unatokana na maelezo tofauti yanayonasibishwa na maana ya historia. ugumu mwingine upo katika namna ya kuendeleza historia, au mtazamo wa anaeifanya historia (mtindo wa kuiendea historia). Hakika hii imesababisha ugumu mwingine ambao ni mabadiliko katika mkondo wa maana ya kuiendea historia kutoka katika mkondo wa kuelezea (descriptive) kuja kwenye mkondo wa uchambuzi (analysis) kutoka kwenye mkondo wa kidini na kuingia katika mkondo wa Kikafiri. Hata hivyo kama mwanafunzi atawapitia wahadhiri wa somo la historia atakuta maana moja kati ya zifuatazo:

i) Historia ni somo la waliyofanya watu, waliyosema na kufikiria.

ii) Historia ni kazi ya kufikiria (ka) ambayo mtunzi anajaribu kuumba maisha na mawazo ya mtu fulani ambae aliishi wakati uliopita.

iii) Historia ni somo linalohusu mambo ya jamii ya mwanadamu yaliyopita na ya sasa.

iv) historia ni ukweli na uhalisia wa maisha ya jamii.

v) Historia ni maelezo juu ya mambo yaliyopita kwa ajili ya muelekeo fulani.

Mawazo haya yanajumuisha mitazamo yote au matapo yote ya historia ya karne ya ishirini ya wanaoielezea historia kwa maelezo ya jumla (kwani matendo yaliyofanywa na watu waliofikiri au kusema hutumia mtazamo wa kusimuliwa) ambao hao wamegawanyika katika matapo au mitazamo (mingi). Wanahistoria wenye mrengo wa kisiasa wanadai mambo muhimu waliyofanya watu kusema na kuwaza yanahusu serikali na sheria. Lipo tapo linalozama kwenye falsafa, sanaa, maandiko na sayansi kama vitu vya msingi katika historia. Wanahistoria wa kiuchumi huzingatia njia zilizowawezesha watu kuishi na kuyamiliki mazingira yao. Kwa wanahistoria wenye mtazamo wa kiutamaduni huzingatia kukua kwa mawazo kwa ujumla ya jamii, siasa na uchumi.

Ama kwa wale wanaochukulia historia kuwa ni maisha ya mtu nao wamegawanyika makundi mawili; wapo wanaodai kuwa wanaweza kutueleza nguvu iliyomsukuma mwanaume au mwanamke kufanya jambo kwa kutumia nadharia ya saikolojia, na wapo wanaokataa nadharia hii.

Kundi la tatu, linaihusisha historia na elimu jamii (sociology) na kuchukulia mambo yaliyopita kama maabara ya kuchunguza mabadiliko ya kijamii yenye manufaa kwa mtazamo wa wakati huu. Tapo hili halimtazami mtu, bali makundi makubwa au jamii. hata hivyo kundi hili nalo limegawanyika, wapo wanaokubaliana na mtazamo wa upembuzi wa kilahidi kwa kuelezea mabadiliko katika jamii na wapo wanaoelezea vingine. Wapo wanaoona kuwa kila jamii ni tofauti na nyingine na wapo Wanahistoria wa sociolojia wanaoona kuwa mifumo ya jamii ilikuwepo kwa jamii zote au inalingana kwa idadi kubwa. Ukizingatia tofauti zote hizi basi historia ni kile ambacho mwanahistoria anakifanya. 1

Maana ya Historia katika Uislamu

Kama ilivyokuwa vigumu kwa mtazamo wa kisekula kueleza maana ya historia kwa maneno mafupi ndivyo hivyo ilivyo katika Uislamu, historia haielezeki kwa maneno machache. Pamoja na ugumu wake, historia katika Uislamu inachukua umbo la kudhihirisha KAULI na mpango wa Mwenyezi Mungu katika kuumba ulimwengu na mwanadamu na malengo ya kuumbwa kwao.

Sema 'OH! mnamkanusha yule aliyeumba ardhi katika siku mbili na mnampa washirika? Huyu ndiye Mola wa Ulimwengu wote. Na akaweka humo milima juu yake. Na akabarikia humo na akakadiria humo chakula chake... katika siku nne. Haya ni sawa kabisa kwa hao wanaouliza. kisha akazielekea mbingu na zilikuwa moshi, basi akaziambia (mbingu) na ardhi "Njooni mkipenda msipende" vyote viwili vikasema tumekuja hali ya kuwa wenye utiifu. (41:9-12).

Enyi watu kama mnashaka juu ya ufufuo (basi tazameni jinsi tulivyokuumbeni) kwa hakika tumekuumbeni kwa udongo (Mzee wenu Adam)) kisha tunakuwa tunakuumbeni nyinyi) kwa manii....." (22:5).

Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake bure. Hii ni dhana ya wale waliokufuru. basi adhabu kali ya moto itawathubutukia wale waliokufuru..... (38:27).

Je, mnadhani ya kwamba tulikuumbeni bure na ya kwamba nyinyi kwetu hamtarudishwa? (23:115).

Na amekutiishiieni vilivyo mbinguni na vilivyomo ardhini vyote vimetoka kwake..... (45:13).

Sikuwaumba majini na watu ila wapate kuniabudu..... (51:56).

Kwa mtazamo huu basi historia pia inaelezeka kuwa ni mpango wa Mwenyezi Mungu katika kuendesha mambo ya mwanadamu kwa mujibu wa lengo la uhai wa mwanadamu na nafasi ya mwanadamu duniani:

(Wakumbushe watu khabari hii) Wakati Mola wako alipowaambia malaika mimi nitaleta viumbe vingine kukaa katika ardhi (wataokuwa Makhalifa wangu) (3:30)

Ili mpango wa Mwenyezi Mungu wa kuendesha maisha ya mwanadamu uwezekane imekuwa lazima Mwenyezi Mungu kutuma Mitume yake pamoja na mwongozo wa maisha.

"Kwa hakika tumewapeleka Mitume wetu kwa dalili waziwazi, na tukateremsha vitabu na uadilifu pamoja nao ili watu wasimamishe uadilifu" (57:25).

Kwa mujibu wa aya hii historia katika Uislamu inapanuka zaidi na kuchukua wajihi wa kumbukumbu zote za Mitume tangu Mtume wa kwanza hadi wa mwisho katika kuwaelekeza Wanaadamu kwa vitendo namna ya kuendesha maisha kwa mujibu wa mpango wa Mwenyezi Mungu. Kutokana na ujumbe huo wa Mitume, Wanaadamu wamegawanyika makundi mawili; kuna walioupokea na kuufuata ujumbe huo hivyo kuwa wasaidizi wa Mitume katika kazi ya kuueneza na kuusimamisha katika maisha yao binafsi na jamii zao; na kuna walioukataa na kuupinga hivyo kuamua kuendesha maisha yao ya kila siku kwa mujibu wa itikadi, mifumo au taratibu walizozibuni ambazo historia inashuhudia kuwa wachache wenye nguvu na mamlaka kwa hila mbalimbali hufaidi rasilimali za ulimwengu huu kupitia migongo ya waliowengi kwa sura ya utawala na utawaliwa bila ya kuwajibika kwa Muumba, ambako kumezaa Shirk iliyosababisha dhulma, ukandamizaji na madhila mengine katika historia ya Mwanaadamu.

Na bila shaka tulimpeleka Mtume katika kila uma ya kwamba "Muabuduni Mwenyezi Mungu na mwepukeni (iblis) muovu." Basi wako miongoni mwao ambao Mwenyezi Mungu amewaongoa na wako miongoni mwao ambao upotofu umethubutu juu yao. Basi tembeeni katika ardhi na mwangalie ulikuwaje mwisho wa wale waliokadhibisha (16:36)

Kwa mtazamo huu basi historia katika Uislamu ni mfululizo wa mapambano na matokeo yake baina ya Uislamu na Ukafiri, haki na dhulma, matendo mazuri na mabaya, wema na uovu, usawa na unyonyaji:

"na wale wanaolipiza kisasi baada ya kudhulumiwa, hao hakuna njia ya kulaumiwa, bali lawama iko juu ya wale wanaodhulumu watu na wakawafanyia jeuri katika ardhi pasipo haki, hao ndio watakaopata adhabu iumizayo. (42:41-42).

Wala msichanganye haki na batili, na mkaficha haki na hali mnajua. (2:42).

Kwa yakini sisi tumekiteremsha kitabu hiki kwa haki, basi muabudu Mwenyezi Mungu kwa kumfanya Mola yeye tu. (39:2).

Kwa namna hii basi tunaweza kusema vile vile historia sio tu ni kumbukumbu ya kazi ya Mitume bali pia ni matokeo ya kazi yao katika kutokomeza kufuru na kusimamisha haki, kusimamisha ufalme wa Mwenyezi Mungu hapa duniani, na kuondoa tawala za Kitwaghuti na shirki.

Safirini katika ardhi na tazameni jinsi ulivyokuwa mwisho wa wale walio tangulia, wengi wao walikuwa wenye kushirikisha. (30:42).

Je, haikuwabainikia watu kama karne ngapi tuliziangamiza kabla yao? Na hawa (makafiri wa sasa) wanatembea tembea katika maskani yao, (hawaoni alama za kuangamizwa kwao). Bila shaka katika haya zimo ishara kwa wenye akili (20:128).

Kwa mujibu wa aya hizi na nyinginezo nyingi zenye maudhui yanayowiana, historia sio kumbukumbu tu au matukio tu bali ni kichocheo cha hoja, dalili, na alama za kuthibitisha kuwepo kwa Mwenyezi Mungu.

Kwa kuzingatia yote haya ni dhahiri kuwa historia ni kuhidhirika kwa mpango wa Mwenyezi Mungu katika kuyaendesha maisha ya mwanadamu, mpango huu ukakamilika wakati wa Utume wa Mtume Muhammad (s.a.w.).

Leo nimekukamilishieni dini yenu, na kukutimizieni neema yangu na nimekupendeleeni Uislamu uwe dini yenu. (5:3).

Kwa kuwa mpango wa Mwenyezi Mungu kusimamia maisha ya mwanadamu umekamilika wakati wa Muhammad (s.a.w.) na kuendesha Dola ya Kiislamu (mpango wa Mwenyezi Mungu katika kuendesha maisha ya wanaadamu) na kwa kuwa Muhammad (s.a.w.) ndio Mtume wa Mwisho, kazi ya kukumbusha na kuusimamisha ujumbe huo imewachwa mikononi mwa Waislamu kwa ushahidi ufuatao:

Nyinyi ndio Ummah bora kuliko zote zilizodhihirishiwa watu, (ulimwenguni) mnaamrisha yaliyo mema na mnakataza yaliyo mabaya na mnamwamini Mwenyezi Mungu... (3:110).

Na wawepo kati yenu wanaoamrisha mema na kukataza maovu..... (3:104).

Ni dhahiri kuwa, historia kwa mtazamo wa Uislamu ni kumbukumbu ya matendo aliyoyafanya mwanadamu kwa kalamu, kauli au vitendo katika harakati zake za kuondoa dhulma na kusimamisha ufalme wa Mwenyezi Mungu hapa duniani iwe mtu mmoja mmoja au kwa pamoja (jamii). Ni kumbukumbu ya mapambano baina ya wanaokandamizwa wakiongozwa na Mitume dhidi ya wakandamizaji (Madhalimu); ni mapambano kati ya wanyonywaji dhidi ya wanyonyaji; watawaliwa dhidi ya watawala:

Na kadhalika tulijaalia kila mji wakuu wao ndio waovu. Ikawa humo wanafanya hila (na vitimbi vya kuzuilia watu na dini ya Mwenyezi Mungu). Wala hawafanyii hila isipokuwa nafsi zao (kwani wanajidhuru wenyewe), lakini hawatambui. (6:123).

Wakasema wale wakuu waliokufuru katika watu wake: "Hakuwa huyu (Nuhu) ila ni mtu kama nyinyi. Anataka kujipatia ubora (umaarufu) juu yenu. Na kama Mwenyezi Mungu angependa (kukufundisheni), kwa yakini angeliteremsha Malaika. Hatukusikia haya kwa wazee wetu wa mwanzo".

"Hakuwa huyu ila ni mtu mwenye wazimu. Basi ngojeeni hata muda (wake atakufa)". (23:24-25).

Na kwa Adi (tulimpeleka) ndugu yao, Hudi Akasema: "Enyi kaumu yangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu; nyinyi hamna Mungu ila yeye. Basi tunakuona umo katika upungufu na tunakuona u miongoni mwa waongo".

Akasema "Enyi kaumu yangu! Mimi sina upumbavu. Lakini mimi ni Mtume niliyetoka kwa Mola wa walimwengu."

"Nakufikishieni ujumbe wa Mola wangu. Na mimi kwenu ni (mtu) nasihi muaminifu:

"Mnaona ajabu kukufikieni mauidha yanayotoka kwa Mola wenu kwa (ulimi wa) mtu aliye mmoja katika nyinyi ili akuonyeni? (Mwabuduni Mwenyezi Mungu) na mkumbukeni alivyokufanyeni makhalifa baada ya watu wa Nuhu. (Mkawa nyinyi washikaji mahala pao). Na akakuzidisheni sana katika umbo. Basi zikumbukeni neema za Mwenyezi Mungu ili mpate kufaulu".

Wakasema (wakuu): "Je! Umetujia ili tumuabudu Mwenyezi Mungu peke yake na tuyaache waliyokuwa wakiyaabudu babu zetu? Basi tuletee unayotuahidi ukiwa ni miongoni mwa wasemao kweli. (Lakini hayo hatuyafuati)". (7:65 -70).

Mtazamo wa Makafiri juu ya Historia

Mtazamo wa Makafiri juu ya Historia unadhihirika vema tukiangalia mtazamo wao juu ya:

(a) Chanzo cha Ulimwengu na asili ya mwanadamu,

(b) Lengo la maisha ya mwanadamu hapa ulimwenguni,

(c) Suala la maisha ya Akhera,

(d) Umuhimu wa kujifunza historia.

(a) Chanzo cha Ulimwengu

Kwa mtazamo wa Makafiri (Wakanao kuwepo kwa Allah (s.w.), chanzo cha ulimwengu, mwanadamu na viumbe vyote kwa ujumla ni maada au jauhari (matter) ambayo haina mwanzo wake wala mwisho wake. Pia makafiri wanadai kuwa uhai (life) umetokana na bahati nasibu (by chance) na hakuna mwanzilishi wake wala mwenye kuuongoza.

Makafiri wanadai vile vile kuwa binadamu ni zao la kiumbe dhalili chenye chembe chembe hai moja tu (unicellular creature) ambacho kilibadilika kutoka katika hali hiyo ya uduni kupitia hatua mbalimbali mpaka kuwa mtu. Kutokana na maelezo yao mtu ni zao la mabadiliko ya kidogo kidgo (Evolution) kutokea kwenye chembe hai moja (Unicellular creature) kisha ikawa samaki (pweza) kisha chura kisha mjusi, nyani (jamii ya manyani) na hatimaye kuwa mtu. Kwa mtazamo wa makafiri mwanadamu hakuumbwa, kwani wao hawaamini kuwepo kwa Mungu Muumba.

Jitihada kubwa sana zimekuwa zikifanyika kueneza nadharia hizi potofu na zimepewa umuhimu mkubwa katika somo la historia mashuleni. Ukirejea kitabu cha Historia cha Shule za Sekondari kiitwacho "Development of African Societies up to the Nineteenth century", kilichoandikwa na Taasisi ya Elimu ya (1981) katika ukurasa wa 11 mwandishi anaeleza kwa muhtasari kuwa:

"Mwanadamu na wanyama wengine wametokea zaidi ya miaka milioni thelathini (30,000,000) iliyopita. Awali mwanadamu alikuwa ni kizazi cha manyani aliishi mitini na kutembea kwa miguu minne kadri siku zilivyopita misitu ilipungua hivyo ikabidi manyani waishi nyikani. Mazingira haya ya wazi yalimlazimisha nyani kusimama kwa miguu miwili ili kuona maadui toka mbali. Hali hii ilimzoesha nyani kutembea kwa miguu miwili. Wakati huo huo anatumia miguu yake ya mbele kuchimbia mizizi na kuchuma matunda. Wakati huo huo akili yake ilikua na kupea zaidi. Hatimaye akatokea mtu tunayemuona leo."

Huu ndio mtazamo wa makafiri juu ya chanzo cha mwanadamu, mtizamo ambao hupandikizwa kwenye vichwa vya kizazi kichanga kila uchao katika somo la historia, biolojia na kemia. Muasisi wa nadharia hii ambayo ilipewa nembo ya mageuzi yenye kuendelea (theory of evolution) ni Bwana Charles Darwin ambaye aliishi zama za utawala wa malkia Victoria wa himaya ya Kiingereza. Hata hivyo utafiti wa kisayansi uliokuja kufanyika baadae ulionyesha kuwa nadharia hiyo si tu haikubaliki kisayansi bali pia haipo katika hakika za kimaumbile zinazoweza kuchunguzika (observable phenomena) kutokana na kasi yake kuwa ndogo mno.

Sayansi mara zote imeelezwa na wanasayansi kuwa haifuati maoni binafsi ya mtu au watu, au visingizio vya kisiasa. Haiegemei upande mmoja, wala haitoi hoja za kujipinga yenyewe bali huzingatia hakika za kisayansi (Scientific facts). Lakini kwa kadiri nadharia ya Evolution inavyohusika, dai hilo laonekana kama si la kweli.

Nadharia ya Darwin imeendelea kufundishwa na kufanywa ndio mtazamo wa wana historia na wanasayansi wa kisekula licha ya ukweli wa kisayansi uliokwishagundulika juu ya asili ya mwanaadamu.

Zaidi kuliko hivyo, maelezo ya Darwin kwamba, aina ya watu wanaoitwa "Homosapien" wametokana na viumbe vilivyopitia mabadiliko mengi hadi kufika hapo, bado hayatupi jibu la Nani aliyeviumba vitu vingi vya ulimwengu huu ambavyo vina hiyo hali ya uwezo wa kimaumbile wa kubadilikka. Kwa sababu zilizokwisha elezwa, "Sayansi" hii haitaki kuzungumzia nani (who) na Kwa nini (why). Inachozungumzia sayansi hii ni Nini (what) na Jinsi gani (how) katika kuyachunguza maumbile mbalimbali ya ulimwengu huu.

(b) Lengo la maisha ya Mwanadamu na hadhi yake hapa ulimwenguni

Kwa mtazamo wa Makafiri mwanaadamu ni mnyama kama wanyama wengine Kinachomtofautisha mwanadamu na wanyama wengine ni ule uwezo wa kupambana na mazingira yake.

Aidha, makafiri wanadai kuwa mwanaadamu hana lengo lolote la maisha isipokuwa lile la kujipatia mahitaji muhimu ya maisha ambayo ni chakula, kivazi na malazi. Kwa mtazamo wao huo, makafiri wanayahusisha matendo yote ya mwanadamu na uzalishaji vitu au uzalishaji mali. Kipimo cha maendeleo kwa mtazamo wa makafiri ni wingi wa mali anayomiliki mwanadamu ambayo hutokana na kuyashinda mazingira yake kwa kiasi kikubwa.

(c) Suala la maisha ya Akhera

Kwanza mtazamo wa makafiri, ulimwenguni na vyote vilivyomo umetokea kibahati nasibu na hivyo hivyo ndivyo utakavyotoweka yaani, makafiri wanadai kuwa hapana Muumba wa ulimwengu na vyote vilivyomo na hakuna maisha mengine baada ya kufa. Mwisho wa maisha ya mtu ni pale anapokufa. Kwa mtazamo wa makafiri, ulimwengu utakuja toweka kama ulivyoibuka kibahati hapo awali. Hivyo wanadai kuwa maisha ya akhera ni jambo la dhana tu lisilokuwa na uthibitisho wowote.

(d) Umuhimu wa kujifunza Historia

Kwa kuwa Historia ni kumbukumbu ya harakati za wanaadamu waliotangulia katika harakati zao za kuzalisha mali, kujifunza historia kwa mtazamo wa kikafiri ni muhimu kwa sababu:

(i) Kunawawezesha makafiri waone ni wapi watu waliopita walifanikiwa na wapi walifeli katika harakati za uzalishaji mali ili wajifunze kutoka kwao. Waige njia zao zilizowapelekea kufanikiwa na wajiepushe na udhaifu wao uliosababisha kufeli kwao.

(ii) Pia historia inasaidia kurekebisha mahusiano kati ya mtu na mtu katika harakati za uzalishaji mali.

2. Mtazamo wa Uislamu juu ya Historia

Kuna tofauti kubwa sana za kimtazamo kati ya Uislamu na Ukafiri juu ya Historia na umuhimu wake. Hili linadhihirika wazi tunapozingatia "chanzo cha ulimwengu na asili ya mwanadamu, lengo la maisha ya mwanadamu, hadhi ya mwanadamu hapa ulimwengu na suala la maisha ya akhera.

(a) Chanzo cha Ulimwengu

Tunafahamishwa katika Qur'an kuwa Muumba wa ulimwengu na vyote vilivyomo ni Allah (s.w.). Hebu turejee aya chache zifuatazo:

"Yeye Allah ndiye Muumba wa mbingu na ardhi pasina ruwaza; na anapotaka jambo basi huliambia tu, "kuwa" nalo huwa. (2:117).

"Bila shaka Mola wenu ni Allah ambaye ameziumba mbingu na ardhi katika siku sita. Kisha akatawala juu ya arshi (yake). (10:3).

(b) Asili ya Mwanadamu na hadhi yake hapa ulimwenguni

Maelezo ya uhakika juu ya asili ya mwanaadamu yamepangwa katika Qur'an tukufu. Mtu wa kwanza mwenye ukamilifu wa kimwili, kiakili na kitabia aliumbwa moja kwa moja na Muumba. Kuumbwa kwake, kuoa kwake, kukosea kwake, kupata kwake msamaha wa Mwenyezi Mungu, kufanywa kwake Mtume, kuja kwake duniani, na juhudi zake za kuitangaza dini ya Allah (Uislamu) ni maelezo yasiyo na shaka au utatanishi.

Hivyo kutokana na mtazamo wa Uislamu asili ya mwanadamu si nyani wala hadhi yake hapa ulimwenguni si sawa na ile ya mnyama. tunafahamishwa katika Qur'an kuwa watu wote ni ndugu wa baba na mama mmoja, Baba Adam na Mama Hawwa. Tunakumbushwa katika Qur'an:

Enyi watu mcheni Mola wenu ambaye amekuumbeni katika nafsi (asili) moja. Na akamuumbia mkewe katika nafsi ile ile. Na akaeneza wanaume wengi na wanawake kutoka katika wawili hao. Na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye kwaye mnaombana. Na (muwatazame) jamaa. Hakika Mwenyezi Mungu ni mlinzi juu yenu (anayaona kila mnayoyafanya).

Enyi watu kwa hakika tumekuumbeni (nyote) kwa (yule) mwanaume (mmoja, Adam) na (yule yule) mwanamke (mmoja, Hawwa). Na tumekufanyeni mataifa na makabila (mbalimbali) ili mjuane (tu basi sio mkejeliane). Hakika ahishimiwaye sana miongoni mwenu mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule amchaye Mungu zaidi katika nyinyi, kwa yakini Mwenyezi Mungu ni mjuzi na mwenye habari (za mambo yote). (49:13).

Kutokana na aya hizi tunajifunza kuwa watu hutokana na kizazi cha Adam (a.s.) na Hawwa na wote ni sawa mbele ya Allah (s.w.) bila ya kujali tofauti za ukoo, ukabila, utaifa au rangi zilizopo. Mwenye hadhi na heshima mbele ya Allah (s.w.) ni yule amchaye ipasavyo.

Pia tunajifunza katika Qur'an kuwa mtu wa kwanza kuumbwa ni Adam (a.s.) ambaye pia alifanywa Mtume wa Allah kwa wanawe. Adamu (a.s.) ameumbwa kutokana na udongo kama tunavyojifunza katika Qur'an:

"Na (kumbuka) Mola wako alipowaambia Malaika: Hakika mimi nitamuumba mtu kwa udongo mkavu unaotoa sauti wenye kutokana na matope meuisi yaliyovunda." "Basi nitakapomkamilisha na kumpulizia roho inayotokana na mimi, basi mumuangukie kwa kumtii." (4:1).

"Na Allah amekuumbeni kwa udongo, kisha kwa tone la manii, kisha akakufanyeni wanaume na wanawake. Na Mwanamke yoyote hachukui mimba wala hazai ila kwa ilimu yake.... (35:11).

Baada ya ya kuzingatia aya hizi ya kwanza ya An-Nisaa (4:1) tuliyoinukuu awali binadamu ni kiumbe aliyeumbwa kutokana na mfinyango wa udongo, kisha akapuliziwa roho itokanayo na Allah (s.w.) kisha akaumbiwa mkewe Hawwa, kutokana na asili hiyo hiyo ya udongo na roho kisha kutokana na wawili hao, uzazi ukaendelea kwa njia ya kawaida tunayoitumia mpaka hivi leo. Ni kwa msingi huu watu ni wana wa Adam au kwa ufupi "wanaadamu" au Binadaamu yaani "bin Adam" (watoto wa Adam).

"(Wakumbushe watu habari hii) wakati Mola wako alipowaambia Malaika mimi nitamleta Khalifa katika ardhi..... (2:30).

Aya hii inatufundisha kuwa Mwanadamu ameletwa hapa ulimwengu ili awe Khalifa wa Allah (s.w.). Kuwa Khalifa wa Allah (s.w.) hapa ardhini ni kusimamisha ufalme wa Allah kwa niaba yake. Kusimamisha ufalme wa Allah (s.w.) ni kusimamisha sheria za Allah katika jamii na kuiongoza jamii kwa mwongozo wake. Ni pale tu mwanadamu atakapokuwa Khalifa wa Allah (s.w.) ndipo atakapoweza kuishi kwa furaha na amani na kulifikia lengo halisi la maisha yake hapa ulimwenguni. Ukhalifa wa Allah (s.w.) si cheo anachojipachika mtu bali atavishwa cheo hiki yule mwenye kumuamini Allah (s.w.) ipasavyo na kufanya vitendo kama mwenyewe Allah (s.w.) anavyoahidi katika Qur'an:

Mwenyezi Mungu amewaahidi wale walioamini miongoni mwenu na kufanya vitendo vizuri kuwa atawafanya Makhalifa katika ardhi kama alivyowafanya Makhalifa wale waliokuwako kabla yao, na kwa yakini atawasimamishia dini yao aliyowapendelea, na kwa yakini Atawabadilishia amani baada ya hofu yao. Wawe wananiabudu hawanishirikishi na chochote. Na watakaokufuru baada ya hayo basi hao ndio wavunjao amri zetu (24:55).

Katika aya hii Allah (s.w.) anaahidi kuwa wale watakaoamini vilivyo kwa kufanya yale yote anayoyaridhia na kuyaacha yale yote aliyoyakataza atawawezesha kuwa watawala katika ardhi watakaohakikisha kuwa sheria za Allah (s.w.) ndizo zinazotawala katika jamii. Hii ni ahadi ya kweli yenye kutekelezwa pasina shaka. Na nani mkweli wa kutekeleza ahadi hii kuliko Mwenyezi Mungu kama ilivyo dhihiri kwa Mtume Muhammad (s.a.w.) na jamii ya Kiislamu aliyoiunda katika kipindi cha miaka 23.

(c) Lengo la maumbile na lengo la maisha ya hapa Ulimwenguni

Mtazamo wa Uislamu juu ya lengo la maisha ya mwanadamu na lengo la kuwepo ulimwengu uliomzunguka ni tofauti na ule wa kikafiri. Mtazamo wa makafiri tumeshauona kuwa ulimwengu huu hauna Muumba na kwa hiyo haukukusudiwa ufikie lengo lolote. Uislamu unatufundisha kuwa, haiwi kwa mwenye akili kukubali kuwa ulimwengu huu na vyote vilivyomo vimekuwepo tu bila ya lengo. Lengo la kuumbwa ulimwengu na vilivyomo limebainishwa katika Qur'an:

Yeye ndiye aliyekuumbieni vyote vilivyomo katika ardhi (kabla hajakuumbeni ili mkute kila kitu tayari) tena akakusudia kuumba mbingu na akazifanya mbingu saba. Naye ndiye ajuaye kila kitu. (2:29).

Na hakika tumekumakinisheni (tumekukalisheni) katika ardhi na tumekuwekeeni humo (vitu vyote) vinavyohitajika katika maisha yenu. Ni shukrani chache tu mnayoshukuru (bali hamshukuru chochote). (7:10).

Kutokana na aya hizi tunajifunza kuwa maumbile yote ya ardhini na angani yaliyomzunguka mwanadamu, anayoyaona na asiyoyaona, yote yako pale kwa ajili ya kumtumikia na kuboresha maisha yake. Ili kufikia lengo hili, Allah (s.w.) amevitiisha vitu hivi kwa Mwanaadamu kwa kuviwekea sheria madhubuti za maumbile (natural laws).

"Na amekutiishieni vilivyomo mbinguni na ardhini, vyote vimetoka kwake (45:13).

Kisha mwanadamu ametunukiwa akili na vipawa vya fahamu na elimu ya kumuwezesha kuyatumikisha maumbile kwa ajili ya kuboresha maisha yake. Maendeleo ya sayansi na teknolojia ni katika jitihada za mwanadamu za kuyatumia maumbile na nguvu kwa ajili ya kuboresha maisha yake.

Kwa kuwa vitu vyote vimeumbwa kwa lengo la kumtumikia mwanadamu, je, mwanadamu ameumbwa kumtumikia nani? Je, lengo la maisha ni kujipatia tu mahitaji muhimu ya maisha, chakula, nguo na malazi kama wanavyodai makafiri? Mbona wanyama nao wanajitosheleza kwa mahitaji haya haya pamoja na kuwa lengo la maisha ya mwanadamu ni ili kutosheleza matashi yake ya kinyama? Hii ni dhana ya makafiri kama Allah (s.w.) anavyotutanabahisha:

"Na hatukuumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake bure. Hii ni dhana ya wale waliokufuru. Basi adhabu kali ya moto itawathubutikia wale waliokufuru. (38:27).

Bila shaka kwa wale wenye akili na busara wanayakini kuwa mwanadamu hakuumbwa tu kwa kuletwa hapa bila ya lengo lolote analotarajiwa na Muumba wake alifikie. Bila shaka mwanadamu atakuwa na lengo la juu zaidi kuliko viumbe wengine hasa kutokana na vipawa vya akili na elimu aliyotunukiwa katika viumbe wengine. Lengo la kuumbwa kwa mwanadamu amelibainisha muumba mwenyewe.

Sikuwaumba majini na watu ila tu wapate kuniabudu (51:56).

Maana ya ibada kwa mnasaba wa aya hii ni kumtumikia Allah (s.w.) katika maisha yetu yote. Kumtumikia Allah (s.w.) kuwa ndiye Bwana (Rabb) wetu pekee; ndiye pekee tunayepaswa tujitiishe kwake kwa unyenyekevu kwa kufuata barabara mwongozo wa maisha aliotuwekea. Utiifu na unyenyekevu wetu kwa Allah (s.w.) utadhihirika pale tutakapopania kwa moyo mkunjufu kumtii Allah (s.w.) katika kuendea maisha yetu yote ya kila siku. Ibada kwa mtazamo huu ina muhusu kila mtu binafsi na jamii kwa ujumla. Ili kila mtu amwabudu Allah (s.w.) katika kila kipengele cha maisha kwa muda wote kwa kuunda dola yenye mamlaka kamili ya kuamrisha mema yanayoleta furaha na amani katika jamii na katika kukataza na kuyatokomeza maovu yanayoleta huzuni na vurugu katika jamii.

Pamoja na lengo hili mwanadamu ametunukiwa akili na vipawa vya fahamu vya kumuwezesha kulifahamu lengo la kuishi kwake kisha akaletewa Mitume na Vitabu kutoka kwa Allah ili kumwongoza. Lakini wakati huo huo akapewa uhuru kamili wa kuamua kufuata lengo au kutolifuata. Hapa ndipo mtihani wake ulipo.

"Kwa hakika tumemuumba mtu kutokana na mbegu ya uhai iliyochanganyika (ya mwanaume na mwanamke) ili tumfanyie mtihani (kwa amri zetu na makatazo yetu) kwa hiyo tukamfanya ni mwenye kusikia na mwenye kuona". (76:2).

"Je, hatukumpa (mtu) macho mawili? Na ulimi na midomo miwili? Na tukambainishia zote njia (iliyo nzuri na iliyo mbaya)? (90:8-10).

(d) Suala la maisha ya Akhera

Kutokana na mtihani huu historia ya mwanadamu haiwezi kuishia katika maisha haya ya hapa ulimwenguni tu, bali haina budi kuendelea kwenye maisha mengine baada ya haya, maisha ya Akhera, ili mwanaadamu avune kulingana na alichokipanda hapa ulimwenguni. Atalazimika mtu kutoa hisabu yake mbele ya Bwana wake ni vipi na ni kiasi gani aliishi kulingana na lengo la maisha yake. Je, aliishi maisha ya kumtii na kumnyenyekea Allah (s.w.) katika kuendesha kila kipengele cha maisha yake au aliishi kwa kumkanusha Allah na kumuasi? Kila mtu atalipwa kwa uadilifu kulingana na utendaji wake hapa ulimwenguni. Tunakumbushwa katika Qur'an:

"Na bila shaka tulimpeleka Mtume katika kila umma ya kwamba muabuduni Allah (s.w.) na mwepukeni mwovu (Twaghuti)". (16:36)

Historia ya Mitume huanzia kwa binadamu wa kwanza Adam. Yeye alikuwa mwanadamu wa kwanza kuletwa duniani na Mtume wa kwanza pia; hii yathibitisha kuwa hapakuwa na kipindi cha historia kilichompitikia mwanadamu bila ya kuwa na mwongozo wa Allah.

Hivyo historia ya Uislamu, kwa kufuata mpangilio wa ujaji wa Mitume ni mwigo wa uyakini wa mageuzi ya jamii na watu wake wote, wema na waovu. Ni Kumbukumbu ionyeshayo kupanuka kwa dini (mfumo wa maisha) ya Allahh na ibada zake; siasa, uongozi, hali ya kijamii, kihisia, na tabia, pamoja na mahitaji mbalimbali. Aidha ni somo linaloonyesha jinsi ambavyo Mtume alivyokidhi mahitaji ya wakati wake, na jinsi alivyowajibika kuwaweka watu sawa katika njia sahihi ya maisha na kuonyesha majaribu na vikwazo alivyopitia kwa ajili ya kufikisha ujumbe wa Allah (s.w.) pamoja na kuonyesha sifa alizokuwa nazo yeye na wafuasi wake.

Hata hivyo historia inayobainishwa na Qur'an inaonyesha kuwa kila alivyokuja Mtume na ujumbe kutoka kwa Allah watu waligawanyika katika (makundi mawili). Wale waliupokea ujumbe na kuufuata na wale walioukanusha na kuleta upinzani. Hali hii ilijitokeza na inaendelea kuwepo kutokana na ukweli kwamba Allah (s.w.) amempa mwanadamu uhuru wa kuamini au kukufuru. Lililo muhimu ni njia ya haki kubainishwa na ya upotofu kubainishwa pia. Ama uchaguzi unabakia kwa mwanadamu mwenyewe.

Uhuru huu wa kuchagua ni mtihani kwa mwanadamu, atakaye chagua njia ya sawa' atakuwa na malipo mazuri mbele ya Allah na atakayefuata potofu makazi mabaya ya motoni itakuwa ndio marejeo yake. Qur'an inatufahamisha:

Kwa hakika tumemuumba mtu kutokana na mbegu ya uhai iliyochanganyika (ya mwanaume na mwanamke) ili tumfanyie mtihani (kwa amri zetu na makatazo yetu). Kwa hiyo tukamfanya ni mwenye kusikia (na) mwenye kuona. Hakika sisi tumemuongoa (tumembainishia) njia (zote) mbili hizi, kuwa hii ndiyo ya kheri na hii ndio ya shari). Basi (mwenye tena atakuwa mwenye shukrani au awe mwenye kukufuru. hakika sisi tumewaandalia makafiri minyororo na makangwa na moto mkali (76:204).

Hakuna kulazimishwa (kuingia) katika dini. Uongofu umeshapambanuka na upotofu. Basi anayemkataa shetani na amwamini Mwenyezi Mungu bila shaka yeye ameshika kishiko chenye nguvu kisichokuwa na kuvunjika. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye kusikia mwenye kujua... (2:256).

Historia yaonyesha kuwa kila alipokuja Mtume na kuondoka, watu waliyaacha mafundisho yake kidogo kidogo na kuyachanganya na upotofu hadi ujumbe ukapotea. Inapofikia hali hii Allah (s.w.) huleta Mtume mwingine kuuhuisha ujumbe wake. Mkondo huu wa historia uliendelea hadi alipokuja Mtume Muhammad (s.a.w.), kufikia kipindi hiki cha historia, haja ya kuja Mtume kila baada ya muda iliondoka. Hii ni kwa sababu Allah alichukua ahadi ya kuhifadhi mwongozo aliokuja nao, yaani Qur'an.

Haki sisi ndio tulioteremsha mawaidha (haya) (hii Qur'an) na hakika sisi ndio tutakaoyalinda (15:9)

Sababu ya pili ya kukatika Utume baada ya Mtume Muhammad (s.a.w.) ni kuwa ujumbe uliokusudiwa uje kwa wanadamu ulishakamilishwa.

"...Leo nimekukamilishieni dini yenu, na kukutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe dini yenu (5:3).

Kuna baadhi ya Mitume walipelekwa kwa watu wa taifa maalumu au nchi fulani lakini tunaona kuwa Mtume (s.a.w.) aliletwa kwa walimwengu wote.

Sema (Ewe Nabii Muhammad): Enyi watu. Hakika mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu nyinyi nyote" (7:158).

Nasi hatukukutuma ila uwe rehema kwa walimwengu wote (21:107).

Hii ndio sababu nyingine ya kufanya haja ya kuja Mtume mwingine baada ya Mtume (s.a.w.) iondoke. Msingi wa hoja hizi ni ukweli kwamba lililo muhimu si kuwepo Mtume kimwili bali kufikisha kwake ujumbe uliokusudiwa. Kwa hiyo kama ujumbe wa Allah (s.w.) upo katika usahihi wake kuwepo kwa Mtume kimwili si hitajio la lazima.

1. Historia ya Nabii Adam (a.s.)

Katika kuingalia historia ya Nabii Adam, kwanza tutaangalia chanzo cha mwanaadamu kwa ujumla kisha tutamuangalia Adam na Hawwa na hatimaye kuangalia historia ya watoto wao wawili.

Kuumbwa kwa mwanaadamu

Mwanadaamu ni Kiumbe aliyeumbwa baada ya viumbe kadhaa kuumbwa. Qur'an inatufahamisha kuwa ulipita muda mrefu kabla ya kuumbwa mwanaadamu.

Hakika ulimpitia Binaadamu wakati mrefu katika dahari, hakuwa kitu kinachotajwa.(76:1).

Kabla ya kumuumba baba yetu Adam, Mwenyezi Mungu alizikusanya Roho zote alizozikadiria kuzipa umbile na silka hii kisha akazichukulisha Ahadi ya utii, kama tunavyofahamishwa katika Qur'an:

"Na (kumbuka) Mola wako alipowaleta katika Wanaadamu kutoka migogoni mwao kizazi chao, na akawashuhudisha juu ya nafsi zao (akawaambia): Je, Mimi siye Mola wenu? Wakasema: Ndiye, tunashuhudia. (Akawaambia Mwenyezi Mungu): "Msije mkasema siku ya Kiyama kuwa sisi tulikuwa tumeghafilika na hayo (hatuyajui)."

Au mkasema, Baba zetu ndio walishirikisha zamani, nasi tulikuwa kizazi nyuma yao, basi utatuangamiza kwa sababu ya yale waliyoyafanya waovu?(7:172-173)

Adam Baba wa wanaadamu wote ameumbwa kutokana na udongo kama aya zifuatazo zinavyobainisha.

Na katika ishara zake (za kuonyesha uwezo wake) ni huku kukuumbeni kwa udongo, kisha mumekuwa watu mnaoenea (30:20).

Kwa hakika tulikuumbeni kwa udongo. (22:5).

(Kumbuka) Mola wako alipowaambia Malaika: "Hakika mimi nitamuumba mtu kwa udongo" (38:71).

Kupuliziwa Roho:

Kukamilika kuumbwa kwa mwanadamu hakuishii katika kukamilika kufinyangwa au mifupa kuvikwa nyama bali hukamilika kwa kiumbe huyo kupewa roho.

Ni kutokana na roho mtu hupata fahamu na uwezo wa kuishi:

(Kumbuka) Mola wako alipowaambia Malaika: Hakika mimi nitaumba mtu kwa udongo. Na nitakapomkamilisha na kumpulizia roho inayotokana na mimi, basi mwangukieni kwa kumtii. (38:71-72).

Roho ndiyo inayomfanya mwanadamu awe hai na kuweza kuvitumia vipawa vyake vya kutambua jema na uovu, kwa kuona na kusikia.

Pamoja na nafasi kubwa iliyonayo roho katika uhai wa mwanadamu, lakini mwanadamu mwenyewe hajui hakika ya roho yake. Hii ni kutokana na elimu ndogo aliyopewa mwanadamu.

Na wanakuuliza habari ya roho. Sema: "Roho ni jambo lililohusika na Mola wangu. Nanyi hakumpewa katika elimu ila kidogo kabisa (17:85).

Baada ya Adamu na Hawa kuumbwa na kupelekwa kuishi Peponi kwa muda na baadae kutolewa humo na kisha kuletwa duniani, ndipo kizazi cha Mwanaadamu kilipoanza na kuenea hapa Ardhini:

".....amekuumbeni katika nafsi moja. Na akamuumba mkewe katika nafsi ile ile. Na akaeneza wanaume wengi na wanawake kutoka katika wawili hao."(4:1)

Kuenea huko ni kwa utaratibu mwingine uliowekwa na Muumba huyo, wa kuongezeka kwa kuzaliwa kupitia hatua kadhaa:

Na kwa yakini tulimuumba mtu kwa tone la manii, (mbegu za uzazi) lililowekwa katika makao yaliyohifadhika. Kisha tukalifanya tone hilo kuwa A'laq, na tukaifanya A'laq kuwa pande la nyama, kisha tukalifanya pande la nyama hilo kuwa mifupa na mifupa tukaivika nyama. Kisha tukamfanya kiumbe kingine. Basi ametukuka Allah mbora wa waumbaji (23:12-14).

Nafasi ya mwanadamu hapa duniani

Nafasi ya mwanadamu hapa duniani na uhusiano wake na Allah (s.w.) imebainishwa tangu yeye mwenyewe hajaumbwa. Tunaona katika Qur'an:

(Wakumbushe watu habari hii) wakati Mola wako alipowaambia Malaika: "Mimi nitaweka katika ardhi Khalifa. Wakasema (malaika) utaweka humo watakaofanya uharibifu humo na kumwaga damu, hali sisi tunakutukuza kwa sifa zako na kukutaja kwa utakatifu wako? Akasema (Mwenyezi Mungu): Hakika mimi nayajua msiyoyajua" (2:30).

Tunaona katika aya hii kuwa mwanadamu amepewa cheo cha Ukhalifa wa Allah (s.w.). Yaani kuwa mwakilishi wa Allah (s.w.) ambaye atakuwa na jukumu la kusimamisha na kuusimamia ufalme wa Allah hapa duniani.

Kwa cheo hiki, mwanadamu si mtawala au mwenye mamlaka huria, Mamlaka na ufalme wote ni wa Allah (s.w.), madaraka aliyopewa ni kusimamia hukumu ya Allah bila ya kuongeza au kupunguza. Aidha hana mamlaka ya kutunga sheria ya kuongoza mambo yake kinyume na ile ya Allah.

Cheo hiki cha Ukhalifa kinamuweka mwanadamu katika daraja la hali ya juu na hivyo basi hatakiwi ajidhalilishe na kujiweka chini ya mamlaka ya yeyote yule kinyume na Allah (s.w.).

Kupewa Elimu Nabii Adam

Mwanadamu hakuanza maisha yake katika hali ya ujinga. Allah (s.w.) baada ya kumuumba baba yetu Adam alimpa elimu juu ya mazingira yake.

Na (Mwenyezi Mungu) akamfundisha (Nabii) Adam majina ya vitu vyote, kisha akaviweka mbele ya malaika na akasema (kuwaambia Malaika) "Niambieni majina ya vitu hivi ikiwa mnasema kweli" (2:32-33).

Hatua hii ya kupewa elimu ni muhimu sana kwani cheo cha Ukhalifa kinafungamana na kutawala na kutumia kila kilichoumbwa na kuwekwa katika ardhi kwa manufaa ya mwanadamu. Bila ya kuwa na elimu sahihi juu ya vitu hivyo mwanadamu hawezi kuvitumia. Ukweli huu wa mwanadamu kupewa elimu kabla ya kuletwa duniani ni hoja dhidi ya makafiri wanaodai kuwa mwanadamu amebuni wazo la kuwepo kwa Mungu Muumba kutokana na ujinga aliokuwa nao juu ya mazingira yake:

...Conceptions of supernatural spiritual being, generally seem to have their justification not of course in any evidence of the senses.... But what is their origin, how did such conceptions arise in the first place? We can certainly not regard such conceptions as being the products, as religion itself tells us of divine revelation or arising from any other supernatural... And such an origin can be traced to conceptions of the supernatural or religious ideas in general which owe ther origin first of all to the helpessness and ignorance of men in face of the forces of nature.*

Tafsiri:

Mawazo ya kuwepo Mungu Muumba kwa ujumla hayatokani na ushahidi wa milango ya fahamu...Lakini ni nini chanzo chake, ni namna gani mawazo haya yaliibuka kwa mara ya mwanzo? Na hatuwezi kukubali eti mawazo haya ni zao la ufunuo au yametokana na Mungu Muumba kama dini zinavyotueleza. Mawazo haya ya kuwepo Mungu Muumba au mawazo ya dini kwa ujumla chanzo chake ni ujinga na kukata tamaa kwa mwanaadamu katika kuyakabili mazingira yake.

Iblis na vitimbi vyake:

Tunasoma katika Qur'an kuwa baada ya Nabii Adam kudhihirisha utukufu wake kutokana na elimu aliyopewa na Allah (s.w.) Malaika na Iblis waliambiwa wamtaadhimishe Adam. Malaika walitii, lakini Iblis alifanya kiburi na kuasi.

Na (wakumbusheni watu khabari hii). Tulipowaambia Malaika: Msujudieni Adam" (yaani mwadhimisheni kwa ile ilimu yake aliyopewa). Wakamsujudia wote isipokuwa Iblis, akakataa na kujivuna, na (tokea hapo) alikuwa katika makafiri (2:34).

Mafundisho makubwa mawili yanayopatikana kutokana na aya hii:

(a) Utii kwa Allah:

Malaika baada ya kupata amri walitii bila ya kuleta mjadala. Allah (s.w.) ndiye Muumba na hivyo mwenye mamlaka ya hali ya juu kabisa. Amri yake haivunjwi na amri nyingine yoyote. Wala hatakiwi mtu asite na kujishauri katika kutekeleza agizo la Allah (s.w.).

(b) Ubaya wa kuwa na kiburi na majivuno:

Mtu huwa na kiburi na majivuno pindi akijiona kuwa yeye ni bora kuliko watu wengine. Iblis alijivuna na kuonyesha kiburi kuwa yeye ni bora kuliko Adam. Hivyo ilikuwa haiyumkini kumtaadhimisha ingawa amri ya kufanya hivyo ilikuwa inatoka kwa Muumba wake!

Zifuatazo ni baadhi ya aya zinazodhihirisha kiburi cha Iblis:

(Mwenyezi Mungu) akasema: "Ewe Iblis: imekuwaje hukuwa pamoja na waliotii? Akasema: Siwezi kumtii mtu uliyemuumba kwa udongo mkavu unaotoa sauti, unaotokana na matope yaliyovunda" (7:32-33).

(Mwenyezi Mungu) akasema: Nini kilichokuzuia kumsujudia nilipokuamrisha? Akasema: Mimi ni bora kulko yeye (Mimi) umeniumba kwa moto naye umemuumba kwa udongo" (7:12).

Akasema (Mwenyezi Mungu) "Basi shuka huko, haikufalii kufanya kiburi humo. (Haya) toka, hakika wewe miongoni mwa wadhalilifu" (7:13).

Kiburi ni katika maradhi makubwa. Na Mtume (s.a.w.) amesema kuwa hataingia peponi mtu mwenye kiburi japo kwa kiasi kidogo kama chembe ya Atom. Iblis alionyesha kiburi mara moja na ikatosha kabisa yeye kufukuzwa katika Rehema ya Allah (s.w.). Ni mara ngapi sisi tunaonyesha kiburi kwa kuzivunja amri za Allah?

Azma ya Iblis kumpoteza Adam

Kutokana na kiburi chake Iblis hakuona uzito wa kosa alilolifanya, hivyo hakuona haja kumuangukia Mola wake kutaka msamaha. Bali alizidi kutakabari na kuona anaweza kuikabili adhabu yha Allah. Kwa hiyo badala ya kuomba msamaha akachukua ahadi ya kumpoteza Adam na kizazi chake.

Akasema "Nipe muda (nisife) mpaka siku watakapofufuliwa (viumbe)". Akasema (Mwenyezi Mungu) "utakuwa miongoni mwa waliopewa muda; (lakini si mpaka wakati huo"). Akasema: "Kwa kuwa umenihukumia upotofu basi nitawafikia kwa upande wa mbele yao na nyuma yao na kuumeni kwao na kushotoni kwao, wengi katika wao hutawakuta ni wenye kukushukuru. Akasema Mwenyezi Mungu: "Toka humo, hali ya kuwa ni mwenye kudharauliwa na mwenye kufukuzwa. Atakayekufuata miongoni mwao, (nitamtia motoni) niijaze jahanam kwa nyinyi nyote" (7:14-18).

Akasema: Mola wangu kwa kuwa umenihukumu kupotea, basi nitawapambia (viumbe vyako upotofu) katika ardhi na nitawapoteza wote. Isipokuwa wale waja wako walio safika kweli kweli. (15:39-40).

Katika aya hizi tunamuona Iblis anachukua ahadi ya kumpoteza mwanadamu. Si kwa njia ya kumteza nguvu bali kwa kumpambia hii dunia akaziona starehe ndogo na fupi za dunia hii ndio bora kuliko kuishi maisha ya Ukhalifa.

Kwa maana nyingine anachukua ahadi ya kumghafilisha mwanadamu na jukumu lake la kuwa Khalifa. Hata hivyo Allah anabainisha katika aya hizo kuwa kwa yule atakayemfuata Iblis basi wote pamoja watajazwa katika jahanam. Ukweli ni kwamba hata Iblis mwenyewe alikiri kuwa hana uwezo wa kumpoteza yule aliye shika barabara mwongozo wa Allah.

"Nitawapoteza wote isipokuwa wale waja wako waliosafika kweli kweli" (15:40).

Kwa hiyo wale watakaoacha kujitakasa kwa kufuata hukumu na maamrisho ya Allah (s.w.) basi hao ndio kundi la Iblis.

Kujaribiwa kwa Adam na Iblis

Qur'an inatufahamisha kuwa baada ya kuumbwa kwa Adam, aliumbwa mkewe Hawwa katika asili ile ile ya Adam. Maelezo zaidi vipi aliumbwa hayakubainishwa ndani ya Qur'an. Bali tunafahamishwa ni kuwa anatokana na asili ile ile ya Adam.

Enyi watu: Mcheni Mola wenu ambaye amekuumbeni katika nafsi (asili) moja. Na akamuumba mkewe katika wawili hao (4:1)

Baada ya kuumbwa wote wawili (Adam na Hawwa) waliwekwa katika bustani, ambapo hakika yake anaijua Allah (s.w.). Walikuwa huru kulia vilivyomo bustanini ila mti mmoja ambao walikatazwa wasiukaribie.

Na tulisema (baada ya hapo kumwambia Nabii Adam): Ewe Adam; kaa wewe na mkeo katika bustani hii; msiukaribie mtii huu tu, msije kuwa miongoni mwa waliodhulumu (nafsi zao kwa kukhalifu amri za Allah) (lakini) shetani (Iblis) aliwatelezesha wote wawili (wakakhalifu amri ile) na akawatoa katika hali ile waliokuwa nayo. tukawaambia: Nendeni hali ya kuwa ni maadui nyingi kwa nyinyi, na makazi yenu (sasa) katika ardhi, na (mtapata) starehe humo kwa muda makhususi. (2:35-36).

Kulingana na mafundisho ya aya hizi wote wawili - Adam na Hawwa walifanya makosa na wakatolewa katika hiyo bustani na Adam na mkewe wakazidi kuonywa kuwa Iblis ni adui kwao hivyo wasimfanye mwenzi wao.

Iblis alipomuasi Mola wake hakutaka kukiri kosa lake na kuomba magh'fira. Bali alizidi kutakabari na akajiweka mbali zaidi na Rehema ya Allah (s.w.). Hali haikuwa hivyo kwa Adam na Hawwa. Baada ya kutanabahi kuwa wamemkosea Mola wao waliomba Magh'fira wakasamehewa.

Kisha Adam akapokea maneno (ya maombi) kwa Mola wake, (akaomba) na Mola wake akapokea toba yake, hakika yeye ni mwingi wa kupokea toba na Mwingi wa kurehemu (2:38).

Na Mola wao akawaita (akawaambia) Je, sikukukatazeni mti huu na kukwambieni ya kwamba shetani ni adui yenu aliye dhahiri? Wakasema: Mola wetu tumedhulumu nafsi zetu, na kama hukutusamehe na kuturehemu bila shaka tutakuwa miongoni mwa wenye khasara (kubwa kabisa) (7:23).

Maelezo ya aya hizi za Qur'an yanafuta zile dhana potofu kuwa kuna dhambi ya asili ambayo kila azaliwaye huirithi.

Adam alikosa lakini alitubia na akasamehewa. Kwa hiyo binadamu huzaliwa akiwa hana dhambi, bali huja kuzichuma mwenyewe kutokana na jinsi atakavyoyaendesha maisha yake.

Kuletwa kwa Adam Duniani

(Wakumbushe watu khabari hii) wakati Mola wako alipowaambia Malaika: "Mimi nitaleta Khalifa kukaa katika ardhi: (2:30).

Hivyo bustani aliyowekwa ilikuwa ni mapito tu Awamu ya kwanza ya maisha ya mwanaadamu ilikuwa ni peponi, awamu ya pili ni maisha ya hapa ardhini awamu ya tatu maisha ya Barzakh (kaburuni) na awamu ya nne baada ya hukumu (Siku ya Kiyama), Mwanzo wa mwanadamu kuishi katika ardhi unabainishwa na aya zifuatazo:

Akasema (Mwenyezi Mungu): "Shukeni (katika ardhi), nyinyi kwa nyinyi ni maadui. Na makao yenu yatakuwa katika ardhi, na starehe yenu (pia) mpaka muda (niutakao mimi mwenyewe).

Akasema (Mwenyezi Mungu): "Mtaishi humo na mtafia humo, na mtatolewa humo (mtafufuliwa kwenda Akhera kulipwa) (7:24-25).

Mwongozo wa Allah kwa Wanaadamu

Allah (s.w.) hakumuacha Khalifa wake aanze maisha gizani. Bali alimpa mwongozo wa namna ya kuutekeleza Ukhalifa wake. Tunasoma katika Qur'an:

Tutakasema: "Shukeni humo nyote, na kama ukikufikieni mwongozo utokao kwangu basi watakaofuata uongozi wangu huo haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika, lakini wenye kukufuru na kuyakadhibisha maneno yetu, hao ndio watakaokuwa watu wa motoni, humo watakaa milele. (238-39).

Utaratibu wa Allah unaobainishwa na aya hizi - wakuleta mwongozo unafanya kazi toka binadamu wa mwanzo Adam hadi wa mwisho wa maisha haya ya duniani. Ni ahadi aliyoichukua Allah (s.w.) kuwaletea waja wake mwongozo. Mwongozo ambao unakusudiwa watu waufuate na ili watu wasibuni mifumo ya maisha kinyume na ule aliouleta Allah (s.w.). Na zipo njia mbili tu za kuujua mwongozo wa Allah. Ama mtu kuletewa Wahyi (Mitume) au kusoma kutoka kwa walioletewa Wahyi. Ndio maana tunaona Allah (s.w.) ameleta Mitume pamoja na vitabu kuubanisha mwongozo huo.

Mwongozo huo umeletwa hatua kwa hatua, hadi kufikia kwa Mtume wa mwisho. Ni mwongozo unaokigusa kila kipengele cha maisha kwa mtu binafsi, Taifa, hata kimataifa ngazi zote katika hali zote, mahali popote na wakati wowote.

Historia ya watoto wawili wa Nabii Adam - Habil na Qabil

Na wasomee khabari za watoto wawili wa Adam kwa kweli, walipotoa sadaka, ikakubaliwa ya mmoja wao na ya mwingine haikukubaliwa Akasema (yule asiyekubaliwa sadaka yake): "Nitakuua". Akasema (yule aliyeahidiwa kuuawa): "Mwenyezi Mungu huwapokea wamchao tu". "Kama utanyoosha mkono wako kwangu kuniua, mimi sitanyoosha mkono wangu kukuuwa. Hakika mimi ninamwongopa Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu pia:

"Mimi nataka ubebe dhambi zangu na zambi zako, na kwa hivyo uwe miongoni mwa watu wa motoni. Na haya ndiyo malipo ya madhalimu."

"Basi nafsi yake ikamwezesha kumwua nduguye, na akawa miongoni mwa wenye kukhasirika.

Hapo Mwenyezi Mungu akamleta Kunguru anayefukua katika ardhi ili amwonyeshe jinsi ya kuificha maiti ya ndugu yake. Akasema: (yule ndugu aliyeua) "Ole wangu: Nimeshindwa kuwa sawa na kunguru huyu na kuficha maiti ya ndugu yangu"? basi akawa miongoni mwa wenye kujuta. Kwa sababu ya hayo tukaawandikia wana wa Israel ya kwamba atakayemuua mtu bila ya yeye kuua mtu, au bila ya kufanya fisadi katika nchi, basi ni kama ameua watu wote, na mwenye kumwacha mtu hai (kumsaidia kuishi) ni kama amewaacha hao watu wote. bila shaka Mitume waliwafikia na hoja zilizo wazi; kisha wengi katika wao baada ya haya walikuwa waharibifu sana katika nchi (5:27-32).

Katika ya hizi majina ya watoto hawa wa Adam hayakutajwa. Bali majina hayo yamechukuliwa kutokana na maandishi mengi ya historia - hasa historia ya Mayahudi. Wafasiri wengi wa Qur'an wanataja katika kuzitafsiri aya hizi kuwa, habil na Kabil ni watoto wa moja kwa moja wa Adam na Hawwa. Na sio imetajwa kwa ishara tu kwa kuzingatia kuwa watu wote wametokana na Adam na Hawwa. Kwa mujibu wa maelezo ya Sheikh A.S. Farsy, hiki ndicho kisa cha awali cha mtu kumuua mwenziwe. Na aliyeuawa ndiye mwanadamu wa mwanzo kufa. Kwa sababu hiyo basi aliyefanya mauaji hakujua nini la kufanya na yule maiti. Ndipo Allah (s.w.) akamleta kunguru kumwonyesha namna ya kuhifadhi maiti ya ndugu yake.

Ili kuyafahamu vyema mafundisho ya kisa hiki cha watoto wa Adam ni vyema tuyazingatie mazingira na wakati ziliposhuka aya za kukielezea kisa chenyewe.

Tunafahamu kuwa awali Allah (s.w.) aliwachagua Mayahudi na kuwapa ujumbe wake ili watekeleze wao wenyewe na kisha waufikishe kwa watu. Kwa hiyo akawatuma Mitume wengi miongoni mwa Mayahudi. Kutokana na neema hii waliyopewa kuletewa mwongozo na kupewa jukumu la kuusimamia, wakawa ni watu wenye hadhi kubwa.

Enyi kizazi cha Israili (Mayahudi); Kumbukeni neema zangu nilizokuneemesheni na nikakutukuzeni kuliko viumbe wengine (wa wakati huo) (2:47).

Hata hivyo Mayahudi hawakuithamini neema hii ila wachache tu. Zaidi ya wao wenyewe kutofuata mwongozo waliwaua Mitume na kufuata baadhi ya kitabu huku wakiacha sehemu nyingine. Hii iliwapelekea kupata laana ya Allah. Aidha, Mayahudi walibashiriwa kuja kwa Mtume (s.a.w.) na waliahidi kuwa watamfuata. Bali alipokuja walimkataa.

Na (wakumbushe) aliposema (Nabii) Isa bin Maryam (kuwaambia Mayahudi); "Enyi wana wa Israil; mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu, nisadikishaye yaliyokuwa kabla yangu katika Taurati, na kutoa habari njema ya Mtume atakayenijia nyuma yangu ambaye jina lake litakuwa Ahmad (Muhammad).

Lakini alipowajia kwa hoja zilizo wazi, walisema: Huu ni udanganyifu ulio adhahiri. (61:6).

Mayahudi hawakuishia kumkataa tu Mtume (s.a.w.) walidhamiria kumua pia. Hapakuwa na jingine lililowapelekea kufanya hivyo, bali ni husuda na kiburi.

Ni katika mazingira haya, Allah (s.w.) anabainisha kisa hiki cha watoto wa Adam ili kuwaonya Mayahudi na sisi sote kuwa: Tusiwe na husuda juu ya Neema na amali njema za watu wengine hata tukaingia kwenye makosa kama ya mtoto wa Adam. Bali nasi tuzitakase nafsi zetu kwa kutenda mema kwa ajili ya Allah (s.w.) nasi atuinue daraja. Allah hawaongoi na kuwapokelea maombi watu madhalimu. Aidha, uongofu haupatikani kwa kumwonea husuda na kijicho mwenye kufanya mema. Bali kwa kujitakasa na kufanya amali njema.

...Akasema (yule asiyekubaliwa sadaka yake): "Nitakuuwa" Akasema (yule aliyeahidiwa kuuawa): "Mwenyezi Mungu huwapokelea wamchao tu" (5:27).

Vile vile Uislamu unatutaka tusiwe ni wenye kulipiza ubaya juu ya ubaya tunaotendewa. Mtu anatakiwa ajitetee na awatetee wengine dhulma inapotaka kufanyika. Lakini asipange kuwafanyia uovu wengine. Bali amwogope Allah na kuishika njia iliyo sawa.

"Kama utanyoosha mkono kwangu kuniua; mimi sitakunyooshea mkono wangu kukuua, Hakika mimi namwogopa Mwenyezi Mungu. Mola wa walimwengu pia". (5:28).

2. Historia ya Nabii Nuhu (a.s.)

Mtume Nuhu alitumwa kwa watu ambao walikuwa wa mwanzo kupotosha mafundisho ya njia sahihi ya maisha ya Nabii Adam. Kutokana na vidokezo vilivyo ndani ya Qur'an na mabaki ya kihistoria (archaelogical remains) hivi leo simulizi za historia zilizopokelewa kutoka kwa wakazi wa kale wa Kurdistan na Armenia zathibitisha pia kauli hii.

Kulingana na mafundisho ya Qur'an, watu wa Nabii Nuhu hawakukana kuwepo kwa Allah na wala hawakuwa wajinga wa ujumbe wa Allah. Lakini mzizi wa upotofu wao ulikuwa shirki. Walimshirikisha Allah (s.w.) na miungu wengine. Upotofu wao huo wa shirki ulizaa maovu mengi katika jamii. Kuliibuka tabaka maalum lililowakilisha miungu wa uongo. Kidogo kidogo tabaka hilo likahodhi nguvu zote za 'Kidini', siasa, na uchumi katika jamii. Wakafanya vizuizi vya kutenganisha watu wa tabaka la juu na chini. Kwa sababu hiyo; machafuko, ukatili (ukandamizaji) na kuanguka kwa maadili, ukaizamisha jamii katika kina cha chini kabisa cha udhalilifu na ufisadi. Ni katika hali hiyo Mtume Nuhu alitumwa kurekebisha hali ya jamii. Aliifanya kazi hii kwa juhudi na subra kubwa. Lakini watawala fisadi katika jamii waliupiga vita ujumbe wake na kuwalaghai watu wa kawaida wasimfuate Nabii Nuhu. Baada ya kufikia mahali pa kukata tamaa ndipo Nabii Nuhu akamwomba Allah awagharikishe waovu wote.

Mafundisho ya Nabii Nuhu

Mafundisho ya Nabii Nuhu yalikuwa na lengo la kuwarejesha watu wake katika utii wa Allah (s.w.). Tunasoma katika Qur'an sura ya 7 aya ya 59 mpaka ya 64:

Tulimpelekea Nuhu kwa watu wake, naye akasema: "Enyi watu wangu; Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna Mungu ila yeye. Hakika mimi ninakukhofieni na adhabu ya siku hiyo iliyo kuu."

Wakuu wa watu wake wakasema:" "Sisi tunakuona umo katika upotofu (upotevu) ulio dhahiri (kwa kutukataza haya tuliyowakuta nayo wazee wetu)" Akasema: "Enyi kaumu yangu mimi simo katika upotofu (upotevu) lakini mimi ni Mtume nitokaye kwa Mola wa Walimwengu wote".

"Je, mnastaajabu kukufikieni mawaidha yanayotoka kwa Mola wenu kwa njia ya mtu aliye ni mmoja katika nyinyi (aliyekuja) ili akuonyeni na ili muogope na ili mpate kurehemewa?"

Walimkadhibisha tu. Basi tukamuokoa yeye na waliokuwa pamoja naye katika jahazi. na tukawazamisha wale waliokadhibisha aya zetu. Bila shaka hao walikuwa watu vipofu. (7:59:64).

Pia katika sura ya 11 aya ya 25-37 tunasoma:

Na sisi tulimpeleka (tulimtuma) Nuhu kwa watu wake (akawaambia): "Mimi kwenu ni muonyaji anayebainisha (kila kitu).

Ya kwamba msimuabudu yoyote isipokuwa Mwenyezi Mungu tu; hakika mimi ninakuhofieni adhabu ya siku (kubwa) hiyo inayoumiza".

Na hapo wakasema wakubwa wa wale, waliokufuru katika kaumu yake: "Hatukuoni ila ni mtu tu sawa nasi; wala hatukuoni ila wamekufuata wale wanaoonekana dhahiri ni dhaifu (wanyonge) wetu; (wamekufuata) kwa dhana ya mawazo tu (bila kukupeleleza vizuri); wala hatukuoni kuwa unayo ziada juu yetu, bali tunakuoneni ni waongo tu".

(Hapo) akasema: "Enyi watu wangu! mnaonaje kama ninayo dalili wazi iliyotoka kwa Mola wangu, na amenipa rehema kutoka kwake (ya Utume), nayo ikakufikieni; je tutakulazimisheni kuikubali ijapokuwa mnaichukia?"

"Na enyi watu wangu; mimi sikuombeni ujira juu ya (jambo) hili; sina ujira wangu ila kwa Mwenyezi Mungu na mimi sitawafukuza walioamini (kama mlivyotaka kwangu niwafukuze hao madhaifu ndipo msilimu nyinyi watukufu. Sitafanya hivyo); maana wao watakutana na Mola wao (awalipe kwa mema yao na mabaya). Lakini mimi nakuoneni nyie ni watu mnaofanya ujinga. (Mnakataa kuifuata haki kwa sababu imefuatwa na madhaifu).

"Na enyi watu wangu; Ni nani atakayenisaidia mbele ya Mwenyezi Mungu; wala kuwa mimi najua mambo ya ghaibu; wala sisemi, "mimi ni malaika," wala sisemi kwa wale ambao yanawadharau macho yenu kuwa Mwenyezi Mungu hatawapa kheri. Mwenyezi Mungu anajua yaliyomo katika nafsi zao.

(Nikisema hivi) hapo bila shaka nitakuwa miongoni mwa madhalimu".

Wakasema: "Ewe Nuhu; umejadiliana nasi na umekithirisha (umezidisha) majadiliano nasi, basi tuletee unayotuahidi, (kuwa tutaadhibiwa); ikiwa miongoni mwa wanaosema kweli".

"Akasema: "Mwenyezi Mungu atayaleta kwenu akipenda,na nyinyi hamtaweza kumshinda."

"Wala haitakufaeni nasaha yangu nikitaka kukunasihini, kama Mwenyezi Mungu anataka kukuacheni kupotea. yeye ndiye Mola wetu; na kwake mtarejeshwa". "Na unda jahazi mbele ya macho yetu (yaani katika hifadhi yetu, hawataweza kukudhuru) na (iwe sawa na) amri yetu (Wahyi tuliokulet ea)wala usinisemeze (kuwasamehe) wale waliodhulumu nafsi zao kwani (sitawasamehe), kwa yakini wao watazamishwa". (11:25-37).

Kama tulivyoona katika utangulizi wetu, kuwa watu wa Nabii Nuhu walizama katika shirk. Na wakuu katika jamii walifanya jitihada kubwa kuwazuia watu na njia ya Mwenyezi Mungu, kwa sababu wakuu wa jamii (watawala) walikuwa mstari wa mbele katika kupinga ujumbe wa Nabii Nuhu, mfumo wa ushirikina uliotawala jamii uliwafanya wao miungu watu wakiwanyonya na kuwakandamiza wengine. Hivyo kufanikiwa kwa Nabii Nuhu ilikuwa ni kuporomoka kwa maslahi yao.

Hivi leo wakuu wa serikali mbali mbali zinazotawala hupiga vita harakati za Uislamu kwa sababu yahofu ile ile waliyokuwanayo machifu wa watu wa Nuhu ya kupoteza mamlaka endapo shirk itaondoka katika jamii na haki kusimama.

Dua ya Nabii Nuhu (a.s.)

Ni katika utaratibu wake Allah (s.w.) kuwa hawaadhibu watu mpaka awapelekee muonyaji. Kazi ya mjumbe ni kuwabainishia njia ya uongofu na njia ya upotevu. Aidha kuwaongoza watu kwa nadharia na vitendo katika kuifuata njia ya uongofu, na watu hupewa muda wa kujirudi. Ikifikia kuwa hakuna tamaa kwamba watu hao watatubia na kurejea katika haki, basi adhabu ya Allah (s.w.) huwajia.

Nabii Nuhu alijitahidi mwisho wa jitihada zake kuwarudisha watu wake kwenye njia ya haki. Lakini wengi wao wakamkadhibisha na kufanya hila kuwazuia wengine wasimwamini. Qur'an yatufahamisha:

Wakasema wale wakuu waliokufuru katika watu wake. "Hakuwa huyu (Nuhu) ila ni mtu kama nyinyi. Anataka kujipatia ubora juu yenu. Na kama Mwenyezi Mungu angependa (kukufundisheni), kwa yakini angaliteremsha malaika. Hatukusikia haya kwa wazee wetu wa mwanzo.

"Hakuwa huyu ila ni mtu mwenye wazimu. Basi mngojeni hata muda (wake atakufa)" (23:24-25).

Pia katika sura ya 11 tunasoma:

(Nabii) Nuhu akasema: Mola wangu; Hakika hao wameniasi na wamewafuata ambao mali yao na watoto wao haikuwazidishia ila hasara. Na wakafanya hila kubwa kubwa (za kubatilisha dini). Na ambao waliwaambia (wafuasi wao); "msiache miungu yenu, wala msiwaache Waddi wala Suwaa wala Yaghutha wala Yauka wala Nasra. (Majina ya waungu wao wa kisanamu). Nao wamekwishapoteza watu wengi, wala wasiwazidishie madhalimu hawa ila kupotea. Basi kwa ajili ya makosa yao waligharikishwa wakainga motoni, wala hawakuwapata wa kuwanusuru mbele ya Mwenyezi Mungu. (71:21-25).

Ilipofikia kuwa Nabii Nuhu hakuwa na tamaa ya kuwarejesha watu wake waliokufuru katika njia ya Allah alimwomba Mola wake.

Na Nuhu akasema: Mola wangu: Usiache juu ya ardhi mkazi wake yoyote katika makafiri. Hakika ukiwaacha watapoteza watu wako (waliotengenea) wala hawatazaa ila (watoto) waovu wenye kukufuru (kama wao).

Mola wangu nighufirie mimi na wazee wangu. Na kila aliyeingia nyumbani mwangu hali yakuwa ni Muislamu, Waislamu wanaume na Waislamu wanawake. Wala usiwazidishie madhalimu ila maangamizo. (71:26-28).

Katika aya nyingine tunasoma:

Kabla yao watu wa Nuhu walikadhibisha nao. Walimkadhibisha mja wetu na wakasema ni mwendawazimu, na akawa anatolewa maneno makali. Ndipo akamuomba Mola wake (akasema): Kwa hakika nimeshindwa, basi ninusuru. (54:9-10).

Kutengeza Safina

Allah (s.w.) aliitikia dua ya mja wake na akamuagiza atengeneze Safina (jahazi) ya kuwaokolea wale wema gharika itakapofika. Habari hizi tunazisoma katika aya zifuatazo:

Basi tulimletea Wahyi ya kwamba: Unda jahazi mbele ya macho yetu na (sawa na) ufunuo wetu. Basi itakapokuja amri yetu, na tanuri (la ardhi) kufurika (kutoka maji) hapo uwaingize ndani yake wawili wa kila namna, (dume na jike) na watu wako, ila usiseme nami juu ya wale waliodhulumu (nafsi zao). Bila shaka wao watagharikishwa (23:27).

Gharika

Kazi ya kuunda Safina ilipokamilika na Nabii Nuhu kuingia humo na wale alioagizwa na Mola wake, gharika ilikuja na kuwaangamiza waliokadhibisha wote. Allah (s.w.) anatufahamisha katika Qur'an:

Mara tukaifungua milango ya mbingu kwa maji yanayomiminika (kwa nguvu kabisa). Na tukazibubujisha chemchem zilizo katika ardhi, na maji (ya juu na chini) yakakutana jambo lililokadiriwa (na Allah). Na tukamchukua (Nuhu) katika ile (jahazi) iliyotengenezwa kwa mbao ma misumari ikawa inakwenda mbele ya hifadhi) yetu. Hii ni tunzo kwa yule aliyekuwa amekataliwa (amekanushwa). Na kwa yakini tuliacha iwe alama. Lakini je, yuko anayekumbuka? (54:11-15).

Kuangamia kwa mtoto waNabii Nuhu (a.s.)

Tumeona nyuma kuwa baada ya kukata tamaa Nabii Nuhu (a.s.) alimwomba Allah (s.w.) awaangamize waovu. Katika kukubaliwa dua yake Nabii (a.s.) alifahamishwa kuwa waovu wote wataangamizwa. Na yeye (Nuhu) asije akamuomba msamaha yeyote katika waovu.

"Na unda jahazi mbele ya macho yetu (na iwe sawa na) amri yetu (wahyi tuliokuletea). Wala usinisemeze (kuwasamehe) wale waliodhulumu (nafsi zao kwani) (stawasamehe) kwa yakini wao watazamishwa." (11:37).

Katika jumla ya watu ambao hawakuamini alikuwa mtoto wa Nabii Nuhu (a.s.) ambaye naye aligharikishwa na maji.

"Akasema (Nuhu); "Hakuna leo wa kulindwa na amri ya Mwenyezi Mungu isipokuwa yule atakaye mrehem (Mwenyezi Mungu): Mara mawimbi yakaingia baina yao na akawa miongoni mwa waliogharikishwa. (11:14-43).

Nabii Nuhu akiwa na uchungu (kama mzazi) kuona mwanae anaangamia, na akikumbuka ahadi ya Allah (s.w.) kuwa atawaokoa watu wa familia yake, alimwomba Allah (s.w.) amwokoe mwanawe. Ahadi ya kuwaokoa watu wa nyumbani (kwake (familia yake) ipo katika aya ya 40 ya sura ya 11. Hata hivyo adhabu hiyo imewabagua (imewatenga) wale wasioamini.

Aya inasema:

Hata ilipokuja amri yetu, na ardhi ikaanza kufoka maji tulimwambia: "Pakia humo (jahazini) jozi moja katika kila (nyama jike na dume) na (wapakie) watu wako wa nyumbani kwako isipokuwa wale ambao imewapitia hukumu (ya Allah). (11:40).

Dua aliyoiomba Nabii Nuhu (a.s.) kumwombea mwanawe najawabu alilopewa inabainishwa katika ayha ifuatayo:

Na Nuhu alimwomba Mola wake (alipomuomba mwanawe anaangamia) akasema: Ewe Mola w angumwanangu ni katika watu wa nyumbani kwangu (mbona anaangamia?) Na hakika ahadi yako ni haki, nawe ni mwenye haki kuliko mahakimu (wote)".

Akasema (Mwenyezi Mungu): "Ewe Nuhu, Huyu si miongoni mwa watu wako. Yeye ni (Mwenye) mwendo usiokuwa mzuri. Basi usiniombe ambayo huyajui. Mimi nakusihi usiwe miongoni mwa wajinga. (Nuhu) akasema: Ewe Mola wangu mimi najikinga kwako nisije kukuomba (tena) nisiyoyajua; na kama hutanisamehe na kunirehemu, nitakuwa miongoni mwa watakaopata hasara." (11:45-47).

Mafunzo kutokana na historia ya Nabii Nuhu (a.s.) na Watu wake

Katika jumla ya magumu aliyoyapata Nabii Nuhu (a.s.) wakati wa kufanya kazi ya Da'awah ni kuteswa kisaikolojia. Alidhihakiwa na kupuuzwa na wale waliokufuru. Aidha alisingiziwa uendawazimu, kuitwa mwongo na kusingiziwa uayari. Kwa yeyote anayehimiza mema na kukataza maovu ni muhimu sana kuyazingatia magumu haya yaliyomkuta Nabii Nuhu (a.s.). Kusimamisha haki katika jamii si kazi nyepesi. Yahitajia jitihada, mapambano na subra kubwa. Tuzingatie kuwa shirk inapotawala wenye nguvu huwanyonya wengine. Hali hii huwafanya wawe miungu watu na kamwe hawatataka kuachia nafasi hiyo. Kwa hiyo ni lazima wenye mwongozo sahihi waikabili shirk katika mtazamo wa kimapambano.

2. Elimu sahihi na yakweli ni ile itokayo kwa Allah (s.w.):

Wapo watu (wasiomuamini Allah) wanaodai kuwa elimu ni ile inayopatikana katika milango ya fahamu tu. Nje ya hapo hakuna kitu. Hawaamini elimu ya Wahyi. Nabii Nuhu (a.s.) alipokuwa anatengeneza jahazi katika mazingira ambayo hayakuwa ya bahari wala ziwa wala mto mkubwa, makafiri walimcheka na kumuona mwendawazimu. Kutokana na milango yao ya fahamu hawakuona wapi jahazi hilo lingetumika. Lakini Nabii Nuhu (a.s.) aliyekuwa na elimu ya wahyi alijua kwanini jahazi litengenezwe na wapi litatumika. Qur'an inatufahamisha:

Na akawa anaunda jahazi, na kila wakimpitia marais makafiri wa umma wake walikuwa wakimcheka na yeye husema: "Kama mnavyonicheka nasi tutakuchekeni kama mnavyotucheka. Karibu hivi mtajua nani itakayemjia adhabu ya kuumiza (kumfedhehesha) na itakayomteremkia adhabu itakayokaa (naye maisha)." (11:38-39).

Makafiri hawakufumbua kitendawili cha jahazi mpaka gharika ilipowakumba. Kwa mujibu wa maelezo haya, la kuzingatia ni kuwa: Japo milango ya fahamu ni zana bora za kupatia elimu lakini ina udhaifu. Elimu pekee iliyoepukana na udhaifu wa milango ya fahamu ni wahyi. Kwa hiyo tunaposoma ujumbe wa Allah (Qur'an) tuzingatie kuwa umeepukana na udhaifu wa aina yoyote. Ni muhimu basi tuuuchukue kwa mazingatio na juhudi kubwa ya kuutekeleza.

3. uhusiano wa damu hauzingatiwi katika mapambano ya haki.

Mtoto wa Nabii Nuhu (a.s.) kuangamia mbele ya macho ya baba yake ni kielelezo kizuri kuwa katika Uislamu imani ndio msingi halisi wa udugu na si damu. udugu wa damu ungekuwa unazingatiwa katika Uislamu bila shaka Allah (s.w.) asingemgharikisha mtoto wa Mtume wake. Lakini tunaona pamoja na uchungu wa Nabii Nuhu juu ya mwanae, anaonywa asimuombee na wala asimuhesabu kuwa yeye ni miongoni mwa watu wake:

"Akasema (Mwenyezi Mungu): "Ewe Nuhu; Huyu si miongoni mwa watu wako Yeye ni (mwenye) kuasi usiwe miongoni mwa wajinga. (11:46).

Fundisho ambalo lipo wazi katika aya hi ni kuwa mtu hupata radhi za Allah kutokana na imani na amali yake mwenyewe. Sio nasaha yake na mtu yeyote. Kwa hiyo wale ambao hutegemea pepo ya Allah kwa kujinasibisha na watu wawadhiniao kuwa watukufu mbele ya Allah, ni bora wachukue hadhari.

Uongofu na hatimae Radhi za Allah hupatikana kwa kufuata mwongozo wa Allah na sio kujinasibisha na kujiegemeza kwa wacha-Mungu walio hai au waliokwisha kufa. Nadharia za uwalii na usharifu ambazo baadhi ya watu huzifuata hazina msingi wowote ndani ya uislamu. Kila anayefuata maamrisho na kuacha makatazo ya Allah ni walii wa Allah. Na kama Nabii Nuhu alivyoshindwa kumwokoa mwanawe asi; walii hana uwezo wa kumwokoa aliyechupa mipaka. Juu ya mawalii wa Allah Qur'an inatufahamisha:

"Sikilizeni vipenzi vya Mwneyzi Mungu (mawalii) hawatakuwa na khofu (siku ya kiyama) wala hawatahuzunika. Nao ni wale waliamini na wakawa wanamcha Mungu (wanafuata amri zake na wanajiepusha na makatazo yake) (10:62-63).

Ushindi lazima kwa waumini

Kuangamizwa kwa watu waliomkadhibisha Nabii Nuhu ni ruwaza njema kwa waumini hasa wanaharakati. Pamoja na magumu mengi atakayopambana nayo muumini, afahamu kuwa hatimaye ushindi ni wake. Aidha Muumini azingatie kuwa Allah anaweza asimletee ushindi hapa duniani au kuwaadhibu makafiri wakati anaona. Lakini jaza bora zaidi ataipata Akhera..Kwa hiyo Muislamu juhudi yake yoyote ile haipotei bure.

Maisha ya Mtume Ibrahim (a.s.)

Mtume Ibrahim (a.s.) alizaliwa Iraq katika mji wa Ur zaidi ya miaka elfu nane iliyoopita. Tukizingatia kuwa Nabii Nuhu na Saleh na wengineo, walitumwa kuleta ujumbe kwa watu maalum, Nabii Ibrahimu anabaki kuwa Mtume wa kwanza kutangaza ujumbe wa Allah kwa walimwengu wote baada ya nabii Nuhu (a.s.). Alizaliwa katika kipindi cha historia ambapo ujahilina shirki ndivyo vilivyotawala maisha ya Watu kiasi kwamba hakuwepo aliyemjua Mungu wa kweli, wachilia mbali kumuabudu. Taifa alimozaliwa Nabii Ibrahimu (a.s.) ndio wakati huo lililokuwa mbele kwa maendeleo ya sanaa. Walizama katika ibada ya masanamu na nyota. Unajimu, uchawi, ramli na tiba zake vikawa maarufu katika jamii.

Kisiasa na kijamii watu waligawika katika matabaka matatu. Walikuwepo makasisi waliochunga Mahekalu na kuongoza ibada za matambiko zilizofanywa na watiifu. Walisimamia mazishi, ndoa na kuchea michezo ya kipuuzi ya kuigiza ili kkuwaeleza watu habari za ghaibu. Kutokana na udanganyifu na hila za makasisi, watu wengi walipmbazikana kudhania makasisi hao wako karibu na Miungu. Hivyo ilijengeka dhana kuwa kuwatend3a wema na kuwatii makasisi humuweka mtu karibu na Mungu. Au kasisi akimuombea dua njema au basi hupata neema ya Mungu, kinyume chake hupata maangamizi. Katika mchezo huu makasisi waliwapumbaza na kuwanyonya raia kwa urahisi kutokana na sadaka za matambiko. Tabaka la pili lilikuwala wakuu wa serikali. Hawa nao waliwanyonya raia kwa msaada wa makasisi. Makasisi walipandikiza dhana katika akili za watu kuwa wakuu wa serikali ni miungu wa dunia hiyo sheria zao ni lazima zitiiwe. Tabaka la tatu ni la raia wa kawaida ambao walinyonywa na makundi yote mawili tuliyotangulia kuyataja. Utagundua kuwa kuna mambo mawili yanayojitokeza katika mfumo huu wa kishirikina; moja, dini kutumika kama chombo cha kuwanyonyea na kuwapumbaza watu. Pili ni ushirikiano unaojitokeza baina ya viongozi wa serikali za kitwaghuti na viongozi wa dini katika kuwakandamiza na kuwanyonya raia. Ni muhimu sana nukta hizi zipambanishwe na jamii yetu ya leo ili kutathmini zinavyofanyakazi na athari zake katika suala zima la kuuzima Uislamu.

Ukoo wa Ibrahimu

Ukoo alimozaliwa Ibrahimu ulikuwa wa makasisi na baba yake alikuwa ndiye mkuu wa makuhani. Kwa hiyo Ibrahimu alikulia na kupata elimu yake katika mazingira ya ukuhani. Aidha cheo cha ukuhani mkuu kilikuwa kinamsubiri akirithi.

Ni vyema tuzingatie kuwa zama hizo jamii nzima ilikuwa imezama katika giza nene la upotofu. Hapakuwa na elimu wala ustaarabu mwingine zaidi ya ule wa kishirikina. Pili, ni kuwa mfumo wa maisha uliwapa nafasi azizi viongozi wa dini, hivyo ilikuwa si jambo la kufikiria kuwa aweza mtu yoyote kuikataa nafasi hiyo. Hata hivyo tunamuona Ibrahimu anakuwa mtu tofauti kabisa na mategemeo ya jamii yake. Allah (s.w.) alimuhifadhi kabisa na machafu ya aina yoyote. Kwa hiyo toka ujana wake alianza kupmbana na mfumo wa maisha wa ushirikina.

Tabia ya Nabii Ibrahimu

Tumeona kuwa Ibrahimu alizaliwa na kulelewa katika jamii ambayo ilikuwa inaongozwa na itidadi ya ushirika. Hata hivyo Ibrahimu alipofikia umri wa kuweza kutumia busara, alianza kutafakari Anajiuliza maswali: Vipi sayari kama nyota na mwezi vyaweza kuwa miungu? Vipi jua laweza kuwa mungu? Vitu ambavyo vyapatikana na kutoweka.Yawezekana vipi masanamu ambayo hayasemi wala kusikia kuwa miungu. Tangu hapo masanamu yenyewe yamechongwa na watu. Vipi mwanadamu apewe sifa ya uungu wakati ana udhaifu mkubwa? Baada ya kutafakari maswali kama haya Nabii Ibrahimu (a.s.) alifikia uamuzi kuwa hataabudumiungu inayoabudiwa na jamii yake akatangaza msimamo wake huo mbele ya watu.

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook