Serikali inatetea dini ipi?

Maaskofu wa Madhehebu ya Pentekoste wamesema kwamba Waislamu wana haki ya kuamini kuwa Yesu sio
Mwana wa Mungu na wala sio Mungu na kuitangaza imani hiyo hadharani.

Wamesema kusema hivyo sio kosa kwani hayo yapo kwenye misahafu yao na kwamba hiyo siyo kashfa dhidi ya Ukristo.

Naye Kadinali Pengo pamoja na Maaskofu wengine na viongozi mbalimbali wa makanisa walishatoa kauli kama hizo.

Aidha viongozi hao wa Makanisa wamesisitiza kwamba Waislamu wanapokosoa Biblia na kusema haifai nayo sio kashfa dhidi ya Ukristo kwasababu kurani imekuwepo ili kuipinga Biblia.

Ni katika kuyazingatia hayo tungependa kuungana na Mheshimiwa Mbunge wa Kigamboni (CCM), Bw. Kitwana
Kondo kuhoji serikali inapomkamata mtu anayemtaka. "Yesu sio Mungu" inaitetea dini ipi? Mbona wenyewe
hawasemi ni kosa? Au tuseme Serikali yenyewe ina dini ambayo inaamini kwamba ‘Yesu ni Mungu?

Kama Serikali haina dini vipi ilani dini moja dhidi ya nyingine!

Itakuwa jambo lisiloeleweka kwa Serikali kusema haina dini huku inawashitaki wanaosema Yesu Si Mungu.

Tunapenda pia tuungane na wale Maaskofu waliolitaka Bunge kubadili sheria na kuweka vifungu vinavyolinda
maslahi ya kuondoa ule utata unaotokana na Serikali kutokuwa na dini.

Lakini lingine pia ambalo lafaa kusisitizwa hapa, ni lile ombi la Maaskofu kwamba Serikali iwaache huru watu wanapohubiri katika maeneo ya wazi; bila kuwajibika kuomba vibali toka Polisi.

Tunaamini kwamba kama Serikali itasimama kwenye katiba na sheria za nchi hapatakuwa na sababu ya kuwa na wasiwasi juu ya amani na utulivu wa nchi yetu.

Machafuko yataweza kutokea pale tu itakapotaka kuyapa madhehebu mengine nafasi bora zaidi na kuyahami
kinyume na maadili ya nchi.