AN-NUUR 
Na.177 Shaaban  1419, Novemba 27 - Desemba 3, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Madini ya chuma 

Na Mujahid Mwinyimvua 

KATIKA moja ya makala zetu za chakula na lishe tuliwahi kuzungumzia dhana ya mlo kamili. Katika makala hiyo tulisema kwamba mlo kamili (balanced diet) ni chakula (mlo) wenye virutubisho vyote muhimu kwa afya ya binadamu (au viumbe wengine). 

Vilevile tulisema kwamba virutubisho hivyo vinaweza kuwekwa katika makundi makuu sita. Makundi hayo ni kabohaidreti (wanga, sukari, nyuzi nyuzi - dietary fibre), mafuta, protini, maji, vitamini na madini. 

Sawiya na hayo, pia tulisema kwamba; kwa ujumla kabohaidreti na mafuta ni virutubisho vinavyoupatia mwili nguvu na joto; protini ni virutubisho vinavyojenga mwili, vitamini ni virutubisho vinavyolinda mwili na, madini na maji ni virutubisho vinavyosaidia kazi zote za hapo juu (kutoa nguvu na joto, kujenga na kulinda mwili). Katika makala yetu ya wiki hii tutatazama chuma kama moja ya madini yanayohitajika mwilini. 

Madini ya chuma (Iron) ni moja ya madini iliyo muhimu watu kuijua, katika nchi zetu za Afrika Mashariki na Kati. Madini nyingine (kwa umuhimu huo) ni madini joto (iodine), ‘zinc’ na ‘fluorine’. 

Chuma ni madini iliyomo katika damu, imeungana na protini katika chembe chembe nyekundu za damu. Muunganiko huo unaitwa ‘haemoglobin’. Haemoglobin inabeba hewa safi (oxygen) kutoka katika mapafu (lungs) na kuipeleka sehemu mbali mbali za mwili zenye chembe chembe hai ili hewa hiyo iunguze chakula na kutoa nguvu na joto. Pia haemoglobin inabeba hewa chafu (carbon dioxide) kutoka katika chembe chembe hai (cells) na kuipeleka katika mapafu, na hatimaye kutolewa nje ya mwili. 

Chembe chembe za damu ambazo huwa na madini ya chuma kama tulivyoona hapo juu, huishi kwa miezi michache. Yaani hufa baada ya miezi michache. Zinapokufa, madini ya chuma kiasi kikubwa hutumika tena kutengeneza chembe chembe za damu mpya. Hata hivyo, kiasi kingine cha madini ya chuma hupotea (hutoka nje ya mwili kwa njia mbali mbali kama mkojo). 

Vile vile, mtu akipoteza damu kwa njia mbalimbali kama vile kujikata, wakati wa uzazi, wakati wa hedhi, kutoa damu hospitalini, n.k., madini ya chuma nayo hupotea kwa wingi. Kama mtu ana kiasi kidogo cha madini ya chuma kuliko mahitaji yake, mtu huyo anapata shida ijulikanayo kama enemia (kupungukiwa damu). 

Tukizingatia maelezo ya hapo juu ni wazi kuwa kila mtu anahitaji madini ya chuma ili mwili wake uweze kutengeneza damu ya kutosha. Ukweli huu uko wazi zaidi hasa katika miaka yetu ya sasa yenye gonjwa la Ukimwi, ambalo mpaka sasa halina tiba wala kinga (ya kitabibu). Ujumbe ninao kusudia kuutoa hapa ni kuwa, watu tujitahidi kuimarisha taratibu zetu za kula ili miili yetu iwe na damu ya kutosha. Hii ni kwa sababu, utakapokuwa na upungufu wa damu, siku hizi (za Ukimwi) kupata damu isiyokuwa na vijidudu vya Ukimwi ni kazi kubwa. Pia uwezekano wa kuwekewa damu yenye vijidudu hivyo upo, hasa tunapoitazama sekta ya afya hapa kwetu Tanzania. 

Katika taaluma (na nyanja nyingine pia) ni mwiko kusema mambo ambayo huna ushahidi nayo. Ninavyoona mimi taarifa ifuatayo inatosha kutoa picha ya sekta ya afya Tanzania, hasa katika kipengele cha tiba. Gazeti la Dar Leo (24/11/1998) likilinukuu gazeti la The African la tarehe hiyo hiyo (24/11/98), limeandika kwamba: "The African lina habari kuwa wafanyakazi wa Hospitali ya Muhimbili wamekiri mbele ya waziri jana kuwa wamekuwa wakipokea rushwa kutoka kwa wagonjwa kutokana na kukatishwa tamaa na mishahara midogo wanayopewa na kufanya kazi katika mazingira magumu. Wafanyakazi hao walimwambia Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Wilson Masilingi, kuwa wamekuwa hawapati mishahara ya kutosha kuendesha maisha yao na vifaa vya Hospitali ya Muhimbili viko katika hali isiyokarabatika". 

Watu ambao miili yao inahitaji kutengeneza kwa wingi chembe chembe nyekundu za damu, ni lazima miili yao hiyo ipate madini ya chuma kwa wingi. Watu hao ni wanawake wanaopata hedhi (siku za mwezi), kinamama waja wazito (wenye mimba), watoto (wanaokua) na watu wenye anemia. 

Madini ya chuma yanapatikana kwa wingi katika vyakula vifuatavyo.:- maini, figo, nyama, maziwa, maharage, nafaka, mboga za majani za kijani kilichokolea), n.k. 

Vyakula kama vile kahawa, chai na nafaka isiyokobolewa zina vitu vinavyozuia mwili kunyonya madini ya chuma kutoka katika vyakula tunavyokula. Hivyo, ni vyema tukapunguza utumiaji wa vyakula hivyo. 
 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 

Tahariri
Hii siyo Demokrasia ni fedheha

Urambo wamlilia Profesa Lipumba
Na Mwandishi Wetu

Sheikh aridhia Waislamu kubatizwa
Na Rajab Rajab, Morogoro

Zanaki kupiga marufuku Hijab?

Uongozi Masjid Qadiria waitwa Polisi kuhojiwa

Wakazi wa Mbagala Msalabani kuishitaki Tume ya Jiji

Wasemavyo wanaharakati

Akhera ipo, makafiri ni wakadhibishaji
Na Abubakar Marwilo

Mdahalo kati ya Waislamu na Wakristo ni mgumu
Na Elia Batendi

Aina ya maudhi yaliyoharamishwa juu ya Muislamu

PAROLE:   Rais kasusa au hana ubavu?
Na Bisura Waziri Nyello

Serikali ikithamini kilimo
Na Abdallah Ahmad Seif

Umuhimu wa Elimu ya Awali kwa watoto wadogo - 3
Na Ustaadh Kupa Pazi Said

Madrasa Arrijalu Muswallin Damba

Ijue Madrasat Fauzia - Kibondo

Waislamu  Kondoa waanza kupokea misaada ya ujenzi wa Msikiti, Madrasa
Na Abu Zubeir, Dodoma

Waislamu Dodoma wasali sala ya Ghaib kwa marehemu Kilima na mkewe

Songea kujenga shule ya sekondari

Wanafunzi wa Bihawana Dodoma wamshukuru Alhaj Ismail Dawood

Mashindano ya kusoma Qur’an yafanyika Kondoa

Waislamu wautazame upya mfumo wao wa elimu

Ujenzi wa Chuo cha Kiislamu Shamsiya Bereko wakwama

Kesi ya kushambulia kituo yaahirishwa tena

Polisi waondolewa kimya kimya Mwembechai

Msikiti wa Kiwanja cha Ndege wapania kujenga shule

Sayansi na Teknolojia
[Kwenye Kompyuta RAM ni kitu gani?]

Mafundisho ya Quran

Masomo ya Dini ya Kiislamu 

Barua za Wasomaji 

Mashairi 

Chakula na lishe 
[Madini ya chuma]

 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita