AN-NUUR 
Na.177 Shaaban  1419, Novemba 27 - Desemba 3, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Akhera ipo, makafiri ni wakadhibishaji
 

Na Abubakar Marwilo 

MWENYEZI Mungu ni mkubwa kuliko wakubwa wote wa bandia ambao wapo katika mgongo huu wa dunia. Zipo sababu ambazo zimekuwa ridhaa kwangu kukiri kwa moyo na kubaini kwa ulimi kwamba Mwenyezi Mungu ni mkubwa na hakuna kama yeye. Ninapenda kutaja moja tu ambayo ni ya msingi kuwa yeye ndie mwanzilishi wa maumbile tunayoyaona na ambayo hatujayaona. Maumbile haya yameumbwa katika kanuni kuu mbili za sheria ya asili.  

Kwa mfano kike na kiume, usiku na mchana, pepo na moto, mvua na ukame, dunia na akhera, na kadhalika. Si nia yangu kuandika somo kuhusu mambo yote haya, bali nia yangu ni kuzungumzia juu ya akhera, yaani maisha baada ya maisha ya dunia hii. 

Kama Mwenyezi Mungu asingeumba akhera, ufufuo na hukumu, Mwenyezi Mungu asingelikuwa mwadilifu kama alivyo hivi sasa. Mwenyezi Mungu ni mwadilifu, hakimu kuliko mahakimu wote. 

Mwenyezi Mungu amewaumba watu na baada ya kuwaumba akawapa madaraka ya kuhusika moja kwa moja na matendo yao. Baadhi yao wanayo tabia ya kufanya matendo mema kama yale yaliyoamrishwa na wengine walio wengi, waume kwa wake wanashindwa kufanya hivyo au wanafanya kinyume kabisa. Katika dunia hii, watu wema wako katika maisha mabaya, na watu wabaya wana maisha mazuri. Watu wasio na makosa yeyote mara kwa mara wanateseka katika mikono ya wanyonyaji na wahalifu. Vivyo hivyo wanyonyaji na wahalifu wanaendelea kuneemeka bila ya hofu ya kuadhibiwa kwa madhambi wanayoyafanya. Polisi, vyombo vya sheria, mahakama, usalama wa ndani na usalama wa Taifa haviwagusi watu hao waovu. Hali hii ni sawa sawa na kuwalinda. Pia inatosha kusema kuwa walimwengu wanapendeleana; hivyo ni vigumu kwao kufanya haki na uadilifu. 

Kama hakuna maisha ya baadaye kuwalipa wafanyao mema na kuwalipa wafanyao mabaya, hakungeweza kuwepo haki. Hakungekuwepo kusudio lolote la kuwaumba watu walio na madaraka juu ya vitendo vyao na kuwatuma Mitume kwao kwa lengo la kuwakumbusha mambo ya Muumba wao. Binadamu ameumbwa kwa lengo maalum; lengo hii si jingine bali ni kumtumikia Muumba wao. Hili pia linawahusu majini. Zipo njia nzuri tu kupitia ili kuwa mtumishi mzuri kupata ridhaa ya Muumba. Ujipinde kwa kutafuta kujua; ujipinde kwa kusikiliza elimu kutoka kwa wajuzi; ujipinde kwa kuwapenda wajuzi au awe mjuzi. Ni mwenye hasara akiwa nje ya mafungu haya. 

Binaadamu walio wengi wa leo wamekuwa wazito kuelewa akhera. Hii inatokana na vitabu wanavyovisoma na itikadi ya maisha yao. Wanadiriki hata kusema kuwa dunia au maumbile yamekuwepo kwa bahati nasibu na Muumbaji hayupo, bali ni fikra tu ya watu. Umaksi umesaidia sana kuwaweka baadhi ya watu katika fikra hizi potofu. 

Fikra hizi potofu si fikra ya zama hizi, bali ni fikra kongwe. Mfalme Pharaoh wa Misri ya wakati ule na watu wengine wengi walikanusha dhana ya Muumba na wao wenyewe wakachukua nafasi ya Muumba. Walijidanganya na hawakufika popote; wakaondoka duniani. Je, Qur’an inatuambia nini kuhusu makafiri hawa wa zama hizo na zama hizi. 

Katika Surat Hajj Aya ya 22 Mwenyezi Mungu anasema: "Na katika watu, wako wanaojadili juu ya Mwenyezi Mungu bila elimu wala uwongozi wala kitabu chenye nuru". Tunajifunza kutokana na aya hii kuwa yule asiyekuwa na elimu, uwongozi au kitabu chenye nuru kutoka kwa Mwenyezi Mungu hawezi kuwa na yakini kuhusu maumbile haya tunayoyaona na tusiyoyaona. 

Upo usemi wa kawaida tu wa Kiswahili unaosema: Msema kweli ni mpenzi wa Mwenyezi Mungu. Ni vyema niseme kuwa miongozo na vitabu vyote vya itikadi vilivyoandikwa na wanafalsafa wa leo na hao wa kale, juu ya mambo ya maumbile na jamii kwa ujumla, vimepitwa sasa na wakati na haviwezi tena kuisimamisha tena jamii katika misingi ya haki, na maisha yao baadae 

Ni Mwenyezi Mungu tu ndie anaweza kutusimamisha sisi katika misingi ya haki, kwani yeye ndie mwanzilishi wa maumbile. 

Mwenyezi Mungu anatuuliza, "Je! anafikiri binaadamu kuwa ataachwa bure?" (75:36). Hili suala ni ngumu kujibu haswa kwa binaadamu asietumia akili. Lakini kwake ni suala lililo rahisi kabisa. Na anatufahamisha bayana katika sura ya 38 Aya ya 27: Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake bure. Hii ni dhana ya wale waliokufuru. Basi adhabu kali ya moto itawathubutikia wale waliokufuru. 

Je, waliokufuru ni akina nani? Kwa tafsiri rahisi ni watu wanaoficha ukweli wa Mwenyezi Mungu. Waliokufuru wamefaulu hapa duniani kujenga tofauti kubwa na mbali mbali za imani na mwelekeo miongoni mwa jamii nyingi. Kila mtu sasa anaitazama dunia hii kwa uoni tofauti tofauti. Hali hii inaashiriya kuwa hakuna anayeweza kuwa hakimu wa mtu yeyote juu ya yupi sahihi na yupi asiyekuwa sahihi. Siku ya ukweli; na siku ya uamuzi ni lazima ifike ili haki na mizanii tendeke kwa binaadamu wote. Uhai wetu ni mtihani; na kifo chetu ni mtihani. 

Baadhi ya watu wanasema akisha kufa, umekufa na hakuna maisha hayo ya baada ya kifo. Hili si kweli kwani linakanushwa na mifano halisi, inayopatikana hapa dunia. Wakati dunia inapopigwa na jua, hufa na akipanda mbegu wakati huo nayo inakufa. Dunia inakuwa hai wakati inaponyeshewa na mvua na ukipanda mbegu wakati huo inaoza na kuchipua mimea mzuri unaopendeza kwa faida ya binaadamu au ya mnyama. Binaadamu hulala wakati wa usiku; anapata mfano wa kifo na baadae kuamka wakati wa mapambazuko; anapata mfano wa ufufuo. 

Akhera ni jambo la uhakika na makafiri wanapoteza wakati wao bure. Mwenyezi Mungu anatufahamisha: Enyi watu! Kama mumo katika shaka juu ya ufufuo, basi kwa hakika tulikuumbeni kwa udongo, kisha kwa manii, kisha kuwa kipande cha damu, kisha kuwa kipande cha nyama kinachoumbika, na kisichoumbika ili tukubainishieni (kudra yetu). Nasi tunakikalisha matumboni tunachokitaka mpaka muda uliowekwa, kisha tunakutoeni kwa hali ya utoto; kisha (tunakuleeni) ili mfikie baleghe yenu. Na kuna wanaokufa. Na katika nyinyi wako wanaorudishwa katika umri dhalili; asijue chochote baada ya kule kujua kwake na unaiona ardhi imetulia kimya lakini tunapoyateremsha maji juu yake, inataharaki na kukua na kuotesha kila namna ya mimea mizuri. Hayo ni kwa sababu Mwenyezi Mungu yuko, na kwamba yeye huwahuisha wafu, na kwamba yeye ni mwenye uweza juu ya kila kitu. Na kwamba kiama kitakuja, hapana shaka ndani yake; na kwa hakika Mwenyezi Mungu atawafufua walio makaburini. (22:5-7). 

Huu ni wakati wa kufanya uchunguzi, kwa sisi Waislamu, ili tuweze kujua wapi tunatoka na wapi tunapokwenda. Pia wakati umefika wa kutengana na watu wenye fikra fupi juu ya maisha na dunia hii. Waislamu hatuna budi kujipanga katika safu za kuamrisha mema na kukataza mabaya kwa ajili ya watu ili kupata akhera bora. Kazi hii ya kuamrisha mema na kukataza mabaya inahitaji kupanga mipango bora na kujitoa mhanga kwa nafsi zetu na mali zetu. Pamoja na hayo yote, tutumie wakati wetu katika mambo ya kimsingi au kinyume cha hivyo tutakuwa hasarani hapa duniani na akhera. 


Mdahalo kati ya Waislamu na Wakristo ni mgumu
 

Na Elia Batendi 

Nimefuatilia kwa makini makala zote nne za Ndugu Nandenga Mkomidachi chini ya kichwa cha habari "Mdahalo kati ya Waislamu na Wakristo." Lengo la makala haya ya Ndugu Mkomidachi kama nilivyomuelewa ni kuwafanya Waislamu na Wakristo wajadiliane, waelewane, na kila mmoja ajifunze imani ya mwingine kupitia njia na rejea sahihi na siyo kuogopana na kujenga chuki zisizo na msingi. 

Katika makala zake, Ndugu Mkomidachi ametaja maeneo kadhaa ya kuyafanyia mdahalo ili yaeleweke kwa wote. Eneo la kwanza kufanyia mdahalo kwa mujibu wa Ndugu Mkomidachi ni UPWEKE WA MUNGU. Ndugu huyu anasema Allah maana yake ni Mungu Mmoja wa walimwengu wote hivyo fikra kya umoja katika Uungu haikubaliki katika Uislamu. Wakristo nao wanaamini MUNGU NI MMOJA aliye na nafsi tatu. Kwa njia ya mkato ni kama umbo la pembetatu ambapo kila kona ina kazi yake lakini bado pembetatu ni umbo moja siyo mambo matatu. Hivyo Wakristo wanaposema nafsi tatu hawana maana ya Miungu Watatu. 

KUTOBAGUA MITUME: Ndugu Mkomidachi anaendelea kueleza kuwa Uislamu unawatambua mitume wote wa Mwenyezi Mungu bila kubagua mmoja wapo. Eneo hili ndilo lenye utata na mdahalo wake ni mgumu kwa sababu Wakristo wanaamini kuwa hakuna Mtume atakayekuja nyuma ya Yesu. Yesu ndiye Alfa na Omega - Mwanzo na mwisho (ufunuo 22:12-13). Pia Mwenye Shamba (Mwenyezi Mungu) alituma watumishi (Manabii) wengi kuwaendea wakulima (walimwengu) wakusanye mavuno lakini watumishi walipigwa na kuuawa, kisha akatuma mwanae, lakini wakulima hao walimuua mwana na kumtupa nje ya shamba (nje ya Yerusalem - Golgotha - Mathayo 21:33-39). Hivyo Wakristo wanaamini Mwenye Shamba (Mungu) ametuma mwana hawezi tena kutuma mtumishi mwingine. Hata hivyo mafundisho ya Kiislamu kuwa hawabagui Mitume yanakosa maana pale wanaposema kwenye shahada kuwa "hapana apaswaye kuabudiwa ila Allah na Mohammad ni mjumbe wake." Hapo tayari ubaguzi umefanyika kwa kuwa mitume wengine hawatajwi. 

KAFARA YADAMU: Ndugu Mkomidachi anaendelea kusema kuwa Allah hana haja na kafara ya damu au Muhanga fulani bali kinachotakiwa ni toba ya kweli, hivyo Waislamu hawaamini ulazima wa kafara. Eneo hili pia mdahalo wake ni mgumu kwa sababu kama Allah hana haja na kafara ya damu, bila shaka Waislamu wanataka kutujenga picha kichwani kuwa Allah ni Mungu Mwingine tofauti na Yehova ambaye alimuagiza Mussa afanye kafara hiyo ya damu ya wanyama (Walawi 5:6) damu ni upatanisho wa Mungu na Wanadamu (Wal. 17:11) Bila damu dhambi haiondoki (Ebrania 9:22). Baadaya Mwenyezi Mungu kuchoka na damu za wanyama alimtoa Yesu achinjwe mara moja tu na damu yake itakuwa ondoleo la dhambi badala ya damu ya wanyama (Mathayo 26:28). Katika toba, damu ni muhimu sana. 

DHAMBI YA ASILI: Ndugu Mkomidachi anaendelea kuandika kuwa dhambi ya asili iliyorithiwa kwa Adamu ni dhana ambayo haikubaliki katika Uislamu kwa kuwa Adamu alitubia na kusamehewa. Hapa mdahalo wake ni mdogo kwa sababu jambo hili liko wazi. Ni wazi Adamu alimkosea Mungu, na adhabu alizopewa zinazotajwa kwenye Biblia Mw. 3:16 kama vile kifo, kula kwa jasho, kuzaa kwa uchungu, shida maradhi n.k. bado tunaendelea kuyarithi. Na kama Adamu alisamehewa baada ya kutubia, bila shaka na adhabu hizi za Adamu tusingerithi, hivyo ni wazi dhambi ya asili ipo. 

ULIPIZAJI KISASI: Bw. Mkomidachi anaandika kuwa Uislamu unahimiza kujilinda na kutokubali kudhulumiwa, hivyo Allah ameagiza Waislamu wawapige wale wanaowapiga ila wasipindukie mipaka. Mkomidachi anaeleza kuwa mafundisho ya Kikristo ya kutojibu mapigo ndiyo yaliyostawisha unyonyaji wa Wakoloni. Eneo hili nalo lina mdahalo mgumu. Lengo la mafundisho ya Yesu kutolipiza kisasi yaliyomo kwenye Mathayo 5:46-47 ni kuonyesha tafauti kwa Mcha Mungu na mpagani? Mbona Mwenyezi Mungu haonyeshi kisasi kwa wasiomwamini kwa kuwa huwanyeshea mvua wabaya na wema. Mafundisho ya ulipizaji kisasi hayana nafasi katika Ukristo. 

Yapo mambo mengi sana ambayo Ndugu Mkomidachi ameyataja kama yanafaa kufanyia mdahalo kama vile ‘Je Kurani’ inategemea vitabu vya kale? Jibu ni ndiyo, asome YUNUS 37. Kuhusu ALHIJR 29 kuwa Malaika ameagizwa kumtii mwanadamu, katika Ukristo hiyo siyo kweli. Kama ni hivyo, basi Malaika Jibril alihalifu amri hiyo pale alipomkaba Nabii Muhammad wakati ameagizwa amtii mwanadamu. Kwa kifupi labda nikubaliane na huyu mwandishi kuwa mdahalo kati ya Waislamu na Wakristo uwe kwa lengo la kufahamiana imani zetu tu kwa sababu tumepishana mambo mengi sana. Kwa mfano mafundisho ya Kiislamu kuwa mbinguni kuna kuoa (ADDUKHAN 54) hayakubaliki katika Ukristo kwa sababu Yesu ambaye anatoka kwa Baba na ajuaye siri za Mbinguni anasema Mbinguni hakuna kuoa wala kuolewa, wote tutakuwa kama malaika (Marko 12:25) Mbinguni ni mahala patakatifu sana, hakuna ulevi kinyume na mafundisho ya Kiislamu kwenye Surat Muhammad 15. Kwa hayo, mwandishi wa Makala hayo aelewe kuwa mdahalo kati ya Waislamu na Wakristo ni mgumu. 

Tunawaomba waandishi wanaokusudia kuchangia hoja ya mjadala, waachane na jazba, ‘ukereketwa’ na pupa. Wawe watulivu na makini ili uwanja huu uwe wa busara na maana kwetu sote. 

MHARIRI. 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 

Tahariri
Hii siyo Demokrasia ni fedheha

Urambo wamlilia Profesa Lipumba
Na Mwandishi Wetu

Sheikh aridhia Waislamu kubatizwa
Na Rajab Rajab, Morogoro

Zanaki kupiga marufuku Hijab?

Uongozi Masjid Qadiria waitwa Polisi kuhojiwa

Wakazi wa Mbagala Msalabani kuishitaki Tume ya Jiji

Wasemavyo wanaharakati

Akhera ipo, makafiri ni wakadhibishaji
Na Abubakar Marwilo

Mdahalo kati ya Waislamu na Wakristo ni mgumu
Na Elia Batendi

Aina ya maudhi yaliyoharamishwa juu ya Muislamu

PAROLE:   Rais kasusa au hana ubavu?
Na Bisura Waziri Nyello

Serikali ikithamini kilimo
Na Abdallah Ahmad Seif

Umuhimu wa Elimu ya Awali kwa watoto wadogo - 3
Na Ustaadh Kupa Pazi Said

Madrasa Arrijalu Muswallin Damba

Ijue Madrasat Fauzia - Kibondo

Waislamu  Kondoa waanza kupokea misaada ya ujenzi wa Msikiti, Madrasa
Na Abu Zubeir, Dodoma

Waislamu Dodoma wasali sala ya Ghaib kwa marehemu Kilima na mkewe

Songea kujenga shule ya sekondari

Wanafunzi wa Bihawana Dodoma wamshukuru Alhaj Ismail Dawood

Mashindano ya kusoma Qur’an yafanyika Kondoa

Waislamu wautazame upya mfumo wao wa elimu

Ujenzi wa Chuo cha Kiislamu Shamsiya Bereko wakwama

Kesi ya kushambulia kituo yaahirishwa tena

Polisi waondolewa kimya kimya Mwembechai

Msikiti wa Kiwanja cha Ndege wapania kujenga shule

Sayansi na Teknolojia
[Kwenye Kompyuta RAM ni kitu gani?]

Mafundisho ya Quran

Masomo ya Dini ya Kiislamu 

Barua za Wasomaji 

Mashairi 

Chakula na lishe 
[Madini ya chuma]

 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita