AN-NUUR 
Na.175 Rajab 1419, Novemba 13 - 19, 1998 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Uchambuzi / Hoja 
Mdahalo kati ya Waislamu na Wakristo- 4
 
Na Nandenga wa Mkomidachi

Katika maelezo yaliyotangulia tumeona pamoja na mambo mengine kwamba theolojia ya Kiislamu inamtazama Mwanaadamu kama ni Khalifa wa Allah hapa ardhini. Kutokana na nafasi hiyo aliyopewa na Muumba wake, atakuwa ni mwenye kujiangamiza na kwa hakika ni kupotoka kwa kiwango cha juu iwapo atajaribu kuyagawa maisha yake pande mbili zinazopingana; ya kiroho na kimwili; siasa au dola na dini. 

Kwa muda mrefu watu wengi wamezielewa vibaya nguzo za Uislamu. Nguzo tano kwa maana ya Shahada, Swala tano, funga , zaka na Hija zimeeleweka kama kaaida za kiroho tu (rituals)

Hata kama zikichukuliwa hivyo bado kaaida hizo, kwa mfano swala inahusisha mambo mengi zaidi ya kuinama na kuinuka. 

Pamoja na hivyo, Uislamu haukomei katika nguzo tano. Nguzo tano ni kama jengo lililosimamishwa mihimili mitano. Lakini lenye kuhitaji vitu zaidi kama vile kuta, dari, milango, madirisha, samani na kadhalika kuupata ukamilifu wake. Kwa hiyo nguzo tano ni lazima lakini zenyewe tu hazikamilishi Uislamu. 

Tukirejea katika kipengele cha swala kwa mfano, tunaweza kuona jinsi kilivyoandamana na mafundisho kadhaa ya kijamii na kisiasa. Hili linamaanisha kutenganisha maisha ni jambo lisilo na nafasi katika Uislamu. Waislamu hawatofautishi kati ya shughuli za kimahitaji na kimaadili. Uadilifu, mambo ya kiroho, kiuchumi, kijamii, Serikali au kiutawala, yote yanahusiana, kwa sababu kila jambo ikiwa ni pamoja na yale ya "kaesari" yako chini ya milki ya Allah na ni yeye pekee anaepaswa kutoa mwongozo. Hili halina budi kufahamika kwa Waislamu wenyewe kwanza. 

Waislamu wanapaswa kujua kwamba kimsingi, Ummah wa Kiislamu unaanza kujengwa kwenye msikiti. Msikiti unapaswa kuendesha shughuli zote. Ndio maana kuna khutba kila Ijumaa, na mara nyingi mawaidha kila baada ya swala. 

Kwa maana hiyo msikiti na jumuiya ya waumini kujifanya kutenganisha "mambo ya imani" na siasa na kinyume chake ni kujikhasirisha, utenganisho huu haukubaliki. na muumini hana ruhusa ya kufanya hivyo. 

Kwa kuwa jumuiya za kidini zinawajibu wa kukemea maovu katika jamii kama vile madawa ya kulevya, rushwa, ujambazi, uasherati (zinaa), utawala mbovu na mzunguko wote wa mambo katika jamii, hazina namna ya kukwepa siasa. Na tangu hapo ni ipi siasa na ipi siyo. Hata kusalimiana na mtu mwingine ni jambo la kisiasa! 

Mahusiano 

Katika kuhitimisha uchambuzi huu unaoangalia uwezekano wa majadiliano kati ya Waislamu na Wasio-Waislamu, hebu tuangalie suala la mahusiano. 

Kwa mujibu wa mafundisho ya Qur’an, kwa Muislamu kulingania ujumbe wa Allah kwa wanaadamu wote ni wajibu kwake. Hili hata hivyo halimaanishi kuwalazimisha watu kuingia Uislamu. Bali kuwakumbusha warejee kwenye Uislamu- dini ya Mitume wote, ambayo imefunuliwa kwa Mtume Muhammad katika muundo wa ukamilisho. Kurejea katika Uislamu ni jambo lenye uzito zaidi kuliko kusilimu. Hatua za kurejea kwenye Uislamu hazimtoi mtu katika asili yake, kwa sababu tangu hapo Qur’an inafundisha kwamba maumbile halisi ya Mwanaadamu yameumbwa yakiwa na silka ya unyenyekevu na utiifu (Uislamu), yamepandikizwa hisia za kumjua Muumba na shauku ya kutaka kumtii, kumnyenyekea na kumuabudu. kwa sababu hivyo Qur’an ina maelezo yafuatavyo:- 

"Hakuna kulazimishwa (mtu kuingia) katika dini. Uongofu umekwisha pambanuka na upotofu. Basi anayemkataa shetani na akamwamini Mwenyezi Mungu, bila shaka yeye ameshika kishiko chenye nguvu kisichokuwa na kuvunjika. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye kusikia (na) Mwenye kujua (2:256). 

Kwa maneno mengine, kumlazimisha mtu ni kinyume na Uislamu kwa sababu dini inategemea, pamoja na mengine, imani madhubuti na matashi ya muhusika, na haya hayaji kwa kulazimishwa. Kwa hivyo kuingia Uislamu si kubadili dini bali kurejea katika njia sahihi kumuelekea Mungu wa kweli ambaye kutokana naye vyote vimeumbwa na kupewa maumbile mbali mbali. Muislamu anafundishwa kuwavumilia wengine. Qur’an imekataza kuwalazimisha watu kuingia katika Uislamu. Pia inakataza kuwalaghai, kuwavamia, kuwashambulia watu kwa lengo la "kuwasilimisha". Kinyume chake unahimiza kujilinda na kutokubali kudhulumiwa. Na hapo ndipo unapoachana na baadhi ya mafundisho ya Biblia ambayo huwakataza waumini wake hata kutetea nafsi zao: 

"Mmesikia kwamba imenenwa, jicho kwa jicho, na jino kwa jino; lakini mimi nawaambia, msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akupigaye shavu la kuume, mgeuzie na la pili. Na mtu atakayekushitaki na kuitwaa kanzu yako, mwachie na joho pia. Na mtu atakayekulazimisha mwendo wa maili moja, nenda naye mbili....." (Mathayo 5:38-41). 

Mafunzo haya ya Biblia badala ya kupiga vita, bila shaka yalistawisha unyonyaji wa kikoloni. Kinyume kabisa na mafunzo ya Biblia, Qur’an inatueleza ifuatavyo: 

"Na piganeni katika njia ya Mwenyezi Mungu na wale wanaokupigeni, wala msipindukie mipaka. Kwani Mwenyezi Mungu hawapendi warukao mipaka. 

Na waueni popote muwakutapo, na muwatowe popote walipo kutoweni; kwani kuwaharibu watu na dini yao ni kubaya zaidi kuliko kuua......(2:190-191). 

Aya hizi hazimaanishi kumpa ruhusa Mwislamu kuchupa mipaka bali zinaelekeza kanuni za kufuatwa na Muislamu anapokabiliana na yule anayemfanyia jeuri. Lakini, hata hivyo "watu wa kitabu" (Ahlul kitab), jina maalumu ambalo Qur’an imewaita Wayahudi na Wakristo, wamepewa nafasi tofauti na wengine. Makundi haya mawili yameitwa "Ahlul Kitab" yametenganishwa na washirikina na makafiri kutokana na kufuata kwao baadhi ya mafundisho ya vitabu vitakatifu vilivyoshushwa kwa Mitume waliopita. Ingawa Waislamu wanaonyesha maeneo ya kitheolojia yenye kasoro au tofauti, kama ilivyofanyika katika uchambuzi huu, lakini bado wanaamini utakatifu wa maandiko hayo kama ulivyokuwa asilia. Kwa hivyo, iwapo mtu wa kitabu ataingia katika Uislamu inafahamika kwamba yeye anarejea baada ya mghafiliko (revertee). Washirikina na makafiri wanapotaka kuwa Waislamu, wao huhitajia kusilimu (converts). 

Baada ya kufahamu hivyo, swali la msingi lililobaki hapa ni namna gani Muislamu anavyotakiwa kuwatendea "watu wa kitabu"? 

Jibu lake linapatikana ndani ya Qur’an: 

Mwenyezi Mungu hakukatazeni kuwafanyia Ihsani na uadilifu wale ambao hawakupigana nanyi kwa ajili ya dini wala hawakukufukuzeni katika nchi zenu. Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wafanya uadilifu. 

Mwenyezi Mungu anakukatazeni na wale ambao wanapigana nanyi katika dini, na kukufukuzeni katika nchi zenu, na wanasaidia katika kufukuzwa kwenu; (Anakukatazeni) kuwafanya marafiki; na wawafanyao, marafiki basi hao ndio madhalimu. (60:8-9). 

Hivi sasa Ulimwenguni kote waumini tunakabiliwa na hatari ya ukafiri, ulahidi (materialism), usekula na kufa kwa maadili. Pia kuna zile za madawa ya kulevya, ugaidi, rushwa, mbinyo wa kisiasa, ubeberu na uchumi kandamizi. 

Matatizo haya yanatuweka waumini kambi moja ambayo inahimiza ushirikiano kukabiliana nayo. Na kushirikiana huko ni katika maagizo ya Qur’an: 

Na kama Mwenyezi Mungu angalitaka angekufanyeni kundi moja, lakini anataka kukujaribuni kwa hayo aliyokupeni. Basi shindaneni kuyafikiia mambo ya kheri. Nyinyi nyote marudio yenu ni kwa Mwenyezi Mungu; Naye atakuambieni yale mliyokuwa mkikhitilafiana. (5:48). 

Ushirikiano ni sharti katika kuuweka Ulimwengu katika haki, uadilifu na amani. Iwapo waovu hushirikiana kufanya uharibifu, iweje watu wema (wanadini) wasishirikiane kuleta ustawi na muruwa Ulimwenguni. 

Kwa hiyo, zipo sababu za kutosha na za lazima zinazohimiza Waislamu na Wasio-Waislamu kukutana, kujadiliana, kuelewana, kushikana mikono na kutembea pamoja kuelekea njia ya kweli, amani na uadilifu; njia ya Allah (s.w.). 

Waislamu na Wakristo kila mmoja ajifundishe imani ya mwingine kupitia njia na rejea sahihi, na si kuogopana kufuatia propaganda za vyombo vya habari. Jamii zote mbili zisitoe fursa kwa maadui kujipenyeza. Jamii moja ya waumini isisaidiane na adui kuinyanyasa, kuikandamiza na kuidhulumu jamii nyingine. Chuki zisizo na msingi zitachochea uhasama na migogoro si vinginevyo. 

Wabillah Tawfiiq 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
Maoni  
Kuvuja kwa mitihani: Tuweni wakweli kwa nchi yetu  

Katibu wa Baraza Kuu  azikwa Dar  
Na Mwandishi Wetu  

Ubabe wa madhalimu kuzimwa:  
Na Mwandishi Wetu  

MACHO YA SHUTUMA  
Na Abu Halima Sa Changwa  

Wazo mpachiko (Programmed mind)  
Na Abu Halima Sa Changwa  

Ta'azia: Abbas Shaaban Kilima 1938-1998  

Wasemavyo Wanaharakati  

Mdahalo kati ya Waislamu na Wakristo- 4  
Na Nandenga wa Mkomidachi  

Siri ya Miujiza  
Na Sheikh Bernard P. Nyangasa  

Umuhimu wa Elimu ya Awali kwa watoto wadogo  
Na Ustaadh Kupa Pazi Said  

Ifahamu Madrasat Ghazal Muslim - Moro  
Na Mussa Ally, Morogoro  

Pamoja na sala, tusimamishe zakah  
Na Abubakari S. Marwillo  

Aina za maudhi yaliyoharamishwa juu ya Muislamu  
Na. Ramla  

Israi na Miiraji ni miujiza  
Mwandishi: Maalim Bassaleh  

Pamoja na ahadi ya Serikali kuzifuta: kesi za mihadhara zaendelea mahakamani  
Na Muhibu Said  

Waislamu Uluguruni  Moro wazama kwenye matambiko  

Imarisheni miradi ya elimu -  Prof.  Mikidadi  
Na Mwandishi Wetu, Dodoma  

Teknologia: Jifunze Kuunganisha Kompyuta (5)  
Na Hassan Omar  

Mafunzo ya Qur'an  
Shetani anawaogopesha wenye mali kutoa  

Chakula na lishe  
[Kansa ya tumbo]  

Matangazo  
 
 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita